Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
AFISA Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki(COSOTA)Doreen Sinare amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita,COSOTA ilipokea jumla ya migogoro 136 na kusuluhisha migogoro 118.
Amesema migogoro 10 kati ya hiyo haikumalizika na ilifunguliwa kesi mahakamani na migogoro 8 inaendelea COSOTA.
Sinare amesema hayo jijini hapa leo Machi 21,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa COSOTA katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita ambapo amesema katika migogoro hiyo, COSOTA imehusika na kesi za hakimiliki 10.
Aidha Sinare amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, usajili wa kazi zinazolindwa na Sheria ya hakimiliki na hakishiriki umeongezeka kwa 70% ambapo kuanzia mwaka 2021 mpaka Februari 2025, COSOTA, imesajili kazi za Sanaa na Uandishi 11,519 na Wabunifu 3,436.
“Katika kipindi hicho, kamati maalumu ya Usajili ndani ya COSOTA inayojihusisha na masuala ya usajili, imefanikiwa kutoa mafunzo na ufafanuzi kuhusiana na hakimiliki kwenye kazi zilizopokelewa kwa idadi ya wabunifu 167.
“Vilevile, imetoa jumla ya vyeti 7,679 vya uthibitisho wa umiliki wa hakimiliki kwa wabunifu waliosajili kazi zao,”amesema Sinare.
Pia amesema kwa mwaka 2021 – 2025, COSOTA imefanikiwa kufanya migao miwili, mgao wa kwanza ambao ulikuwa ni mgao wa 23 ulifanyika tarehe 28/01/2022 na ulikuwa wa kiasi cha shilingi 312,290,259,000, ambapo Wasanii 1,123 walinufaika, na ulitokana na matumizi ya kazi 5,924 za muziki ambazo zilitumika katika vituo 11 vya redio.
Mgao wa pili uliofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita ulifanyika tarehe 21/07/2023 na ulikuwa ni mgao wa 24 wa mirabaha kwa kazi za muziki. COSOTA iligawa kiasi cha shilingi 396,947,743.20 na wasanii wa muziki 8,165 walinufaika kupitia kazi zao 61,490.
“Hivyo ni viwango vikubwa zaidi kuwahi kufanyika katika migao ya mirabaha ambayo COSOTA imekuwa ikigawa kwa miaka ya nyuma kabla ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ambao ulianzisha kampeni ya kusisitiza watumiaji wa kazi za Sanaa katika maeneo ya biashara kulipia matumizi ya kazi hizo.
“Uongozi wa Dkt. Samia umefanya mageuzi makubwa ya kibajeti kwa COSOTA kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi kwa kutoa fedha za serikali kiasi cha shilingi bilioni 1.5,”amesema.
Pamoja na hayo amesema katika kuhakikisha tasnia ya hakimiliki nchini inaimarika, COSOTA imepata ufadhili wa mradi wa Mpango wa Kuwezesha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) unaosimamiwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya wenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara.



More Stories
Wananchi waaswa kutoa taarifa vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu
Mvua ilioambatana na upepo yasababisha maafa Kata ya Namanyere
Tanesco,Kanona wakutana kwa mazungumzo ya awali ya biashara ya mauziano ya umeme