Na Mwandishi Wetu
KUONGEZEKA kwa idadi wa wagonjwa walioambukizwa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19) hapa nchini kumefanya mchakato wa kuiuza timu ya Mawenzi Market ya Mkoani Morogoro kuwa mgumu.
Awali viongozi wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ilitangaza kuiuza timu hiyo kwa dau la Shilingi milioni 100, lakini baadaye waliweka wazi kuwa huenda dau hilo likapungua ili kufanikisha kupatikana kwa mteja atakayeinunua.
Sababu za kuwepo uwezekano mkubwa wa kupungua kwa dau hilo ni kutopata mteja aliyetaka kuinunua zaidi ya wale wanaopiga na kuulizia baadhi ya taratibu muhimu zitakazowawezesha kumiliki timu hiyo.
Katibu wa timu hiyo, Juma Kilangiro ameliambia Majira kuwa, licha ya kuweka wazi nia yao ya kutaka kupunguza bei endapo kama kweli atajitokeza mnunuzi, lakini bado hadi sasa hali ipo vilevile kwani watu wengi wanawaambia kuwa watajitokeza baada ya janga hili kumalizika.
Kilangiro amesema kuwa, hadi sasa bado wanaendelea kupokea simu nyingi za wadau wale wanaoulizia taratibu za manunuzi ili kuweza kuwasilisha kwa viongozi wao kuangalia kama wanaweza kuinunua klabu hiyo.
Amesema, miongozi mwa wadau wanaoulizia taratibu za kununua timu hiyo wanatoka katika makampuni ya ndani na nje ya mkoa huo.
“Hadi sasa tumeshaanza kupokea simu kutoka kwa wadau mbalimbali wanaoulizia taratibu za manunuzi ya timu ambao wengi wao wanatoka katika makampuni ambapo pia wamesema kwa sasa hawawezi kwenda kufanya nao mazungumguzo hadi pale hali itakapokuwa shwari. Jambo kubwa kwa sasa ni kusubiri kuona kama tutakubaliana katika manunuzi,” amesema Kilangiro.
Wakati wanatangaza kwa mara ya kwanza kuuza timu hiyo, viongozi hao walisema kuwa, matatizo ya kushindwa kuendesha timu hiyo yalianza muda mrefu lakini walikuwa wakipata msaada sehemu mbalimbali na kuweza kuendesha timu ikiwemo kucheza mechi zao za ndani na nje jambo lililofanya wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia.
Pia wanakabiliwa na madeni mengi ambayo yamewaweka matatani na muda wowote huenda baadhi ya viongozi wakafikishwa mahakamani kutokana na kushindwa kuyalipa.
Miongoni mwa madeni yanayowakabili ni zaidi ya Sh. milioni 18 kwa ajili ya kulipa stahiki za wachezaji wao lakini pia wana deni la zaidi ya Sh. milioni 25 ya pango la nyumba waliyokuwa wakikaa wachezaji wao.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM