March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

COPRA yawaasa wafanyabiashara wa mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko kufuata sheria

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Irene Mlola, amewaasa wafanyabiashara wa mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko kuhakikisha wanajisajili rasmi na mamlaka hiyo ili waweze kufanya biashara zao kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali, hivyo kupata fursa ya kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi kwa njia halali.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 6,2025 katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam,  alisema kuwa biashara yoyote ya nafaka na mazao mchanganyiko isiyofuata sheria ni ukiukwaji wa taratibu, na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kukiuka masharti hayo, ikiwemo kufungwa kwa biashara husika.

“Tunawaasa wafanyabiashara wote wa mazao ya nafaka na mchanganyiko kujisajili COPRA ili waweze kufanyabiashara kwa uhuru, kwa mujibu wa sheria na kupata kipato halali,biashara isiyo rasmi ni hatari kwa uchumi wa mfanyabiashara na taifa kwa ujumla,” alisema Mlola.

Ameeleza kuwa licha ya kuwa COPRA ni taasisi changa yenye miaka miwili tangu kuanzishwa kwake, tayari imeshaanza kushiriki maonyesho ya Sabasaba kwa mara ya pili, jambo linalowapa fursa ya kukutana ana kwa ana na wafanyabiashara wanaotaka kujua zaidi kuhusu taratibu za kuendesha biashara za mazao hayo kwa ufanisi.

 Mlola alifafanua kuwa katika banda lao, wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya watu wanaokuja kuuliza namna ya kujisajili, kupata vibali vya biashara na jinsi ya kushiriki kwenye masoko ya kimataifa kupitia bidhaa wanazozisimamia.

 “Tunawaelekeza hatua kwa hatua jinsi ya kujisajili ili waingie rasmi kwenye mfumo. Hii inawarahisishia kuingia kwenye masoko ya nje, na kupitia COPRA tunaweza kuwasaidia kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa taifa,” aliongeza.

Aidha, alieleza kuwa COPRA imejipanga kuhakikisha mazao ya nafaka na yale mchanganyiko, ambayo kwa muda mrefu hayakuwa na msimamizi rasmi, sasa yanapata uangalizi wa karibu, hali itakayosaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na kuwapatia wakulima na wafanyabiashara mapato zaidi.

 “Wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi wameonyesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika sekta hii. Kupitia COPRA, tunawasaidia kupata vibali vya usafirishaji na kuhakikisha wanazingatia vigezo vyote vya kimataifa,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliwahimiza wananchi wote na wadau wa sekta ya kilimo kufika katika banda la COPRA ili kujifunza fursa zilizopo na namna ya kujiinua kiuchumi kupitia biashara ya mazao hayo.

“Huu ni wakati sahihi kwa Watanzania kujifunza, kujisajili, na kutumia fursa hizi ili kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa letu,” alisisitiza