Na Joyce Kasiki, TimesMajira,Online Dodoma
SHIRIKA linaloangazia Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto la Children in Crossfire (CIC) limepanga kuzifikia shule za msingi 700 zilizopo katika mkoa wa Dodoma katika utekelezaji wa Mradi wa Watoto Wetu Tunu Yetu.
Mradi huo unalenga kuboresha elimu ya darasa la awali kwa kushirikiana na Serikali na wadau katika mikoa husika.
Akizungumza jijini hapa kuhusu shughuli zinazofanywa na Shirika hilo katika kikao kilichowakutanisha wadau wanaotoa huduma ya elimu msingi ulioandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ,Meneja wa Mradi huo kutoka CIC, Frank Samson amrsema, hivi sasa shirika hilo linatekeleza mradi huo katika mikoa mitatu kwa kushirikiana na mashirika wenyeji.
Ametaja mikoa hiyo na mashirika wenyeji kwenye mabano kuwa ni Mwanza (TAHEA), Morogoro (CDO) na Dodoma (Maarifa ni Ufunguo) .
“Kwa mkoa wa Dodoma ni wilaya za Kongwa na Chamwino ,tulianza mradi na shule za mfano 58 mwaka 2020 na kwa mwaka 2021 tumeweza kuzifikia shule zote 232 katika wilaya hizo.” Amesema Frank
Aidha amesema kwa mwaka huu mradi huo umeweza pia kuzifikia shule 92, katika mikoa ya Morogoro na Mwanza na mpango wao ni kuzifikia shule zote za mikoa hiyo.
Frank amesema,shughuli zinazofanywa katika mradi huo wa Watoto Wetu Tunu Yetu ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wa elimu ya awali, kuboresha mazingira ya kujifunzia,kutoa mafunzo ya uongozi wa elimu kwa ngazi mbalimbali, Kuboresha miundombinu kwa kujenga vyumba vya madarasa na vyoo ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita jumla ya vyumba 30 vya madarasa vimekamilishwa ujenzi wake na vingine 50 vikiwa kwenye mpango.
“Aidha jumla ya vyumba 324 vya madarasa ya elimu ya awali vimekarabatiwa ndani ya mwaka 2020/21,ambapo sambamba na uboreshaji wa madarasa, mradi umeweza kushirikiana na jamii kuweka mifumo ya maji shuleni ili kuhamasisha watoto kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.” Alisema
Aidha amesema mradi umeimarisha ushirikiano wa shule na wazazi ambao umechangia upatikanaji wa lishe Kwa baadhi ya shule, ufuatiliaji wa ujifunzaji wa watoto shuleni na nyumbani, Elimu ya jinsia pamoja na ulinzi wa mtoto.
“Mafunzo ya walimu wa awali yanalenga kupata walimu bora wa Elimu ya Awali, kuongeza umahiri wa ufundishaji, kutengeneza na kuendeleza mazingira ya kujifunza Kwa kutumia vifaa vilivyopo kwenye mazingira ili kuchochea utoaji wa Elimu bora ya Awali Kwa Watoto.” amesisiza Frank
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi