Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) ambacho ni Chuo Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichopo makutano ya Barabara ya Taifa na Chang’ombe katika Kitalu Na.324 na 325 Karibu na Uwanja wa Mkapa (Zamani Uwanja Mkuu wa Taifa), kimeipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua na inazoendelea kuchukua katika kukabiliana na ugonjwa wa corona unaotishia maisha ya watu na uchumi wa nchi.
Akizungumza katika Mahafali ya 14, Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Prof. Stephen Oswald Maluka, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeonesha juhudi za kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutoa miongozo mbalimbali kwa watanzania juu ya namna ya kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.
“Ninapenda pia kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa hatua alizozichukua na anazoendelea kuchukua katika kukabiliana na ugonjwa huu unaokatisha maisha ya watu na kudidimiza uchumi wa nchi na dunia nzima. Shukurani nyingi kwa viongozi katika Wizara ya Afya jinsi wanavyoendelea kupambana katika kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa salama” amesema Profesa Maluka.
Aidha, Profesa Maluka ameishukuru serikali kwa kuendelea kukiwezesha Chuo ikiwemo kukipatia fedha za kuendesha shughuli mbalimbali huku akimuhakikishia Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwamba fedha zote Chuo inazopewa na serikali zitatumika kwa matumizi ya Chuo na endapo itadhihirika fedha hizo kutumika kinyume na matarajio, Baraza la Chuo halitosita kuwachukulia hatua kali wahusika kwani ni kinyume na sheria.
“Chuo kilipata shilingi milioni 950 kutoka Serikalini kwa mwaka wa fedha 2020/2021, kwa ajili ya kuendelea kukarabati majengo na miundombinu ya Chuo. Tunaishukuru sana
Serikali kwa kuendelea kukiwezesha Chuo kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabili. Aidha, tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kukipatia Chuo fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikumbukwe kwamba ni kutokana na msaada wa Serikali, Chuo kimeweza kukamilisha utekelezaji wa Mradi wa Upanuzi wa jengo la Utawala” amefafanua Prof. Maluka
Akitaja mafanikio ya Chuo hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja Profesa amesema Chuo kimefanikiwa kusomesha idadi kubwa ya wafanyakazi wanataaluma na waendeshaji ili kuhakikisha kuwa wanafikia viwango vya elimu vinavyotakiwa. Amesema kwa ajili ya wanafunzi mafunzo ya watumishi Chuo kilitenga shilingi 413,500,000/= huku shilingi 113,500,000 ikitengwa kwa mafunzo ya muda mfupi na shilingi 300,000,000 kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu. Na amebainisha kuwa jumla ya watumishi 54 wanatarajia kunuifaika na mafunzo hayo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Kuhusu changamoto Profesa amesema Chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa ya usomeshaji wa wanataaluma ili wafikie kiwango cha Ph.D, uhaba wa vyumba vya kufundishia na kujifunzia, maktaba za TEHAMA zenye vifaa vyote muhimu na ofisi za watumioshi wa Chuo, pamoja na uhaba wa mabweni kwa wanafunzi wa Digrii za awali ambapo chuo kina jumla nafasi 328 za bweni kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya usimamizi Chuo Kishiriki cha Eliimu Dar es salam Profesa Wlliam A. L. Anangisye amesema wahitimu wana wajibu wa kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19 ili kusiweze kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji mstaafu Damian Lubuva amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeonesha juhudi za kupambana na ugonjwa wa UVIKO 19 ikiwa ni pamoja na kutoa miongozo mbalimbali kwa Watanzania juu ya namna ya kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote