Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaani Institute of Judicial Administration (IJA) kimesema kuwa kimekuwa kikizalisha wanafunzi mahiri wa sheria, ambao wamekuwa na tija kubwa hapa nchini.
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha IJA, Tundonde Mwihomeke akiongea katika banda la chuo hicho kwenye maonesho ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Sradi (NACTVET) ya mwaka 2023 Jijini Arusha, amesema kuwa ufundishaji kwa njia ya mfumo wa umahiri na kuwapeleka wanafunzi wao kufanya mafunzo kwa vitendo mahakamani kumewafanya wawe na ujuzi na utendaji mzuri katika muktadha wa sheria.
“Chuo chetu kinawafundisha wanafunzi kwa mitaala ya kisasa ya umahiri, tunaita competence-based, tunahakikisha mwanafunzi anafundishwa darasani na kupelekwa mahakamani ili kupata ujuzi wa kivitendo, hali hiyo imesaidia sana chuo chetu kuzalisha wanafunzi bora,” amesema Tundonde.
Ameongeza kuwa wanafunzi wanaomaliza chuoni hapo wamekuwa wakifanya vizuri wanapokwenda ngazi za juu za elimu ya sheria, akitolea mfano wa mwanafunzi bora wa Mzumbe ngazi ya shahada mwaka jana kuwa alitokea IJA.
Pia, Tundonde amebainisha kuwa chuo hicho kinaendelea kupitia miongozo yake ya ufundishaji ili mwanafunzi aendane na soko la sasa la sheria na aweze kujiajiri na kuajiriwa.
“IJA huwa na kawaida ya kupitia miongozo yake ya ufundishaji, lengo ni kumfanya mwanafunzi wetu amalize na kuweza kufit (kufaa) soko la ajira, na kuweza kujiajiri mwenyewe,” amebainisha Tundonde.
Chuo cha IJA (Institute of Judicial Administration) kinatoa mafunzo ya sheria kwa ngazi ya stashahada na astashahada, pia kinafanya utafiti wa kisheria na mafunzo kwa wadau wanaojihusisha na masuala ya haki na sheria.
Nae Afisa Udahili wa chuo cha IJA, Magdalena Mlumbe amesema kuwa chuo kina miundombinu muhimu na ya kisasa ikiwemo maktaba, ambayo ina vitabu muhimu katika maarifa ya sheria.
“Chuo chetu kina miundombinu ya kisasa ambayo ni muhimu katika ufundishaji, mathalani kuna maktaba ya kisasa yenye vitabu vya sheria, ambavyo si rahisi kuvipata kwenye maktaba zingine,” amesema Magdalena.
Vilevile, Magdalena ameongeza kuwa chuo kina miundombinu yote muhimu ikiwemo huduma ya malazi, zanahati na viwanja vya michezo.
Kwa upande wake, Ahmed Shemle ambae ni mhitimu wa zamani wa chuo hicho cha IJA, aliyefika katika banda hilo, amesema kuwa elimu ya sheria aliyoipata kutoka chuoni hapo imemsaidia sana kwenye masuala masuala mbalimbali.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi