January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere chaibuka mshindi wa tatu kwenye maonesho ya wiki ya ubunifu

Na Rose Itono, timesmajira

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) kimeibuka mshindi wa Tatu kitaifa katika Maonesho ya Wiki ya Ubunifu Kitaifa 2023, maonesho ambayo yamefanyika katika viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati akifunga Maonesho hayo ya Wiki ya Kitaifa ya ubunifu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo amekipongeza Chuo kwa ushindi huo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof Shadrack Mwakalila, amewapongeza Washiriki wote kwa kuonesha jitihada ya dhati, ambapo ameahidi kuwa bunifu zote zitaendelezwa na kuhakikisha zinatatua changamoto katika jamii.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo hicho Prof Richard Kangalawe amesema chuo kinajivunia ubunifu wa teknolojia mpya ya kuvua samaki kwa kutumia roboti.

Amesema teknolojia hii imelenga kuwasaidia wavuvi kutotumia muda mwingi kutafuta mahali samaki walipo

Aidha mwanafunzi wa Chuo hicho ambaye amebuni teknolojia hiyo Mcha Makame Mcha alisema ametumia miaka miwili kubuni teknolojia hii

“Teknolojia hii itatumia mfumo wa GPS na utajiendesha wenyewe ambapo ukifika sehemu ambapo Kuna samaki utatoa taarifa,”alisema Mcha na kuongeza kuiomba serikali na Wadau wengine kuugikisha ubunifu huu uweze kuingia sokoni.

Maonesho hayo ya Ubunifu yalianza Aprili 24, 2023 na yamehitimishwa leo Aprili 28. Kauli mbiu ya maonesho ilikuwa “Ubunifu kwa Uchumi Shindani.”