Na Esther Macha, Timesmajira Online, Chunya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imesema inaendelea kuwafuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi watakaobainika kuzembea kusimamia elimu ya watoto wao kwa kuwazuia kwenda shule au kuwatumikisha kwenye mashamba ya tumbaku na shughuli za uchimbaji madini.
Hatua hizo zitachukuliwa kuanzia katika Mabaraza ya Kata hadi Wilaya kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Kauli hiyo ilitolewa Januari 11, 2026 na kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Athumani Bamba, ambaye pia ni Mwanasheria wa halmashauri hiyo, alipokuwa akizungumza na Timesmajira kuhusu wajibu wa wazazi kufuatilia elimu ya watoto wao mara baada ya kufunguliwa kwa shule.

Bamba amesema hatua hiyo inalenga kutekeleza maagizo ya Serikali ya kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kuanza masomo, hususan waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, wanapata elimu bila vikwazo.
“Tutahakikisha tunafuatilia maeneo yote, hata ya wafugaji. Tayari tumewasogezea shule karibu na makazi yao, hivyo mzazi hatakuwa na sababu ya kumzuia mtoto kwenda shule. Tutahakikisha hakuna mtoto anayebaki nyumbani,” amesema
Ameongeza kuwa mwaka huu halmashauri imeweka msisitizo mkubwa wa kutumia sheria dhidi ya wazazi watakaokiuka makusudi wajibu wao na kusababisha watoto kuacha shule ili kufanya kazi za kilimo au uchimbaji wa madini, wakati Serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha miundombinu ya elimu.
Bamba amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika miundombinu ya elimu, ikiwemo uboreshaji na usajili wa shule shikizi katika maeneo ya pembezoni kwa jamii za wakulima na wafugaji, ni miongoni mwa sababu zitakazowabana wazazi wazembe.
Aidha amesema kupitia mapato ya ndani, halmashauri imeboresha na kusajili shule shikizi tisa katika maeneo ya pembezoni ili kuondoa adha ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
“Wilaya ya Chunya ina shule 90, kati ya hizo tatu ni za watu binafsi na 87 ni za Serikali. Kati ya shule za Serikali, shule shikizi ni tisa ambazo tayari zimeboreshwa na kusajiliwa ili kupokea wanafunzi na kupelekewa walimu,” amesema
Akizungumzia suala la chakula mashuleni, Bamba amesema halmashauri imeweka utaratibu wa kuchangia Sh1,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kupitia mapato ya ndani, ili kuboresha huduma ya chakula na kuinua kiwango cha taaluma.
Aidha, amesema zaidi ya Sh milioni 450 zimechangwa kuimarisha Mfuko wa Maendeleo wa Chunya unaohusisha wadau wa kilimo cha tumbaku na uchimbaji wa madini ya dhahabu, kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu wilayani humo.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Chunya, Lukelo Mng’on’go, amesema kwa mwaka 2026 jumla ya wanafunzi 4,132 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, huku wanafunzi 41 wakipangiwa shule nje ya wilaya hiyo.
“Tunawahamasisha wazazi kuhakikisha ifikapo Januari 13, mwaka huu, watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti shuleni bila kisingizio chochote, ikiwemo ukosefu wa sare,” alisema.
Naye Kaimu Ofisa Elimu Awali na Msingi Wilaya ya Chunya, John Gwimile, amesema jumla ya watoto 12,478 wameandikishwa kuanza elimu ya msingi, kati yao wavulana ni 6,207.
Ameongeza kuwa halmashauri, kwa kushirikiana na Serikali Kuu, imejenga mabweni kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, ambayo tayari yamekamilika na kuanza kutumika.
“Tunaendelea kupokea watoto wengine wenye mahitaji maalum ili waweze kupata haki yao ya elimu,” amesema.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi