November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chumvi yenye madini joto inayoepusha kupata mtoto bubu,kiziwi

Na   Aveline  Kitomary,TimesMajira Online,Dar es Salaam

MADINI  joto (iodine) ni kirutubishi muhimu kinachohitajika kwenye mwili wa binadamu,huhitajika kwa kiasi kidogo hivyo  mtu anatakiwa kupata madini joto kila siku .

Kutokana na uhitaji wa kila siku madini hayo ni sehemu ya chakula.

Binadamu anahitaji madini joto kiasi cha kijiko kimoja tu cha chai kwa maisha yake yote.

Kwa wastani mtu mzima anahitaji kiasi cha mikrogramu 100-150 kila siku japo mahitaji kwa wajawazito ni makubwa zaidi  hadi mikrogamu  175.

Madini joto hupatikana katika ardhi na binadamu huyapata kwa kula vyakula vinavyopatikana  kwenye ardhi hiyo  kiasi cha madini hayo hutegemea wingi wa madini hayo ardhini.

Hata hivyo maeneo ya miiniko na milima huwa na kiasi kidogo cha madini joto kwani yanakuwa yamepotea kutokana na kuchukuliwa kwa maji.

Hivyo ili kuhakikisha madini joto yanatumiwa na kila mtu yanachanganywa katika chumvi ili kuhakikisha watu wengi wanayapata kutokana na chumvi kutumika kila siku.

Hii imefanya sheria ya matumizi ya chumvi kuanzishwa na kupishwa na Bunge mwaka 1994 ili kusimamia na kuhakikisha  kuwa chumvi yote inayozalishwa na kuingizwa nchini kwa matumizi  inakuwa inachanganywa  na madini joto.

Sheria hiyo ni kifungu  katika sheria  kuu ya madini  ya mwaka 1976 na ile ya chakula ya mwaka 1978 na vifungu vivyo vimefanyiwa mapitio mwaka 2003 na kuwa kanuni mwaka 2010.

Taasisi ya chakula na lishe  kwa kushirikiana na wadau wa chumvi  ilisambaza mashine za kupima kiasi cha madini joto kwenye chumvi kwa halmashauri zote  zinazozalisha chumvi.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dk Germana Lyena. anasema  wamekuwa wakifatilia  mara kwa mara  uongezwaji wa madini joto kwa wazalishaji  na wauzaji wa chumvi katika maeneo mbalimbali.

“Hata hivyo kwa kushirikiana na wadau tulifanya mapitio ya  mkakati wa uongezwaji madini joto kwenye chumvi na kubainsha changamoto zilizopo.

“Tulibaini uwepo wa wazalishaji wa chumvi wengi wadogo wadogo  na wa kati katika maeneo ambayo hayafikiki kiurahisi na wenye kuzalisha chumvi isiyo bora.

“Mapendekezo yaliyotolewa  ni kuandaa miundo mbinu inayowajumuisha wazalishaji chumvi wadogo ,wa kati na wakubwa ,kufanya utafiti wa kina  ili kupata maelezo ya kina  ili kuongeza ufanisi na uzalishaji wa chumvi bora,”anabainisha Dk Lyena.

TAKWIMU ZILIVYO NCHINI

Upungufu wa madini joto ni  moja kati ya matatizo ya lishe nchini tangu miaka ya 1980.

Tatizo hili ni tatu kwa ukubwa katika matatizo ya lishe  ikilinganishwa na tatizo mengine ya udumavu ,uzito pungufu ,upungufu  wa wekundu wa damu na upungufu wa vitamin A.

Tatizo hili linaathiri afya na maendeleo ya jamii ikiwa ni pamoja na uzalishaji mali na uchumi.

Takwimu za kitaifa za matumizi ya chumvi yenye madini joto zinaonesha kuwa kaya zinazotumia chumvi yenye madini hayo zimeongezeka kutoka asilima 90 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 96.4.

Aidha kaya zinazotumia madinin joto toshelevu zimeongezeka kutoka asilimia 47 kwa mwaka 2010  hadi kufikia asilimia 61 kwa mwaka 2015  huku malengo ikiwa ni kufikia asilimia 80  ya kaya kwa mwaka 2021.

UKOSEFU HUSABABISHA KUPUMUA KWA SHIDA.

Mtu anapokosa madini joto ya kutosha mwili hushindwa kutengeneza homoni za tezi za shingo(thyroid hormones) hivyo kufanya uvimbe katika shingo ujulikano kama ‘ goitre’.

“Endapo patakuwa na upungufu au kukosekana  kwa madini joto tezi hilo litachochewa kufanya kazi ya ziada  ya kutengeneza kichocheo  hicho na hatimaye kuongezeka ukubwa.

“Uvimbe wa tezi la shingo unaweza kuwa mkubwa kiasi cha kubana njia ya chakula  na kufanya mtu kupaliwa au kumeza chakula kwa shida ,uvimbe huo pia unaweza kuziba njia ya hewa  na kusababisha mtu kupumua kwa shida,”anasema Afisa lishe mtafiti Anna John.

MTOTO ANAWEZA KUHARIBIKA UBONGO

Upungufu wa madini joto kwa mjamzito huenda kuathiri moja kwa moja ukuaji wa kiumbe kilichopo tumboni .

 Mtafiti lishe huyo  anasema Athari zinatokana na upungufu wa madini hayo kwa mjamzito ni pamoja  na mtoto kuzaliwa na mtindio wa ubongo ,kuwa kiziwi au bubu, mimba kuharibika, na mtoto kuzaliwa kabla ya wakati(njiti).

“Athari zingine ni mtoto kuzaliwa na uzito pungufu ,mtoto kufa akiwa mchanga mtoto kuzaliwa na ulemavu wa viungo, mtoto kuzaliwa akiwa mfu na kudumaa kwa mwili na utaahaira.

“Hali hiyo pia huweza kusababisha mtoto kuchelewa katika hatua za ukuaji na maendeleo ,ugumu katika kuelewa ,kutenda na kufundishika ,kuchelewa kubalehe au kuvunja ungo,”anasema Anna.

Anasema ni muhimu mama kabla ya kushika ujauzito kuwa na madini joto ya kutosha ili kuweza kuaepusha madhara yatokanayo na ukosefu wake.

YANAVYOMFANYA MTOTO KUZINGATIA MASOMO

Umuhimu wa madini  joto wakati wa ujauzito husaidia katika ukuaji  wa mtoto tumboni  ikiwa pia ni kuzuia ulemavu  wa akili  na mwili .

Vile vile  hufanya ukuaji wa mtoto kuwa mzuri baada ya kuzaliwa ikiwemo wakati wa mabadiliko ya kimwili kama vile wakati wa kuvunja ungo au kubalehe.

Kwa mujibu wa Anna , madini hayo yanaweza  kuongeza uwezo wa kuelewa ,kutenda na kufundishika hii ni baada ubongo kupata madini joto ya kutosha.

“Asilimia 90 ya ukuaji wa ubongo unatokea kati ya wiki tatu ya mimba mpaka miaka miwili  baada ya kuzaliwa  hivyo kwa kila hatua ya ukuaji madini joto yanahitajika ili kuepuka madhara ,”anaeleza.

MADHARA YA CHUMVI NYINGI

Daktari wa Lishe Esta Nkubi anasema  matumizi makubwa ya chumvi ni hatari katika mwili kutokana na Sodium ambayo inaweza kusababisha seli za mwili kuvuta maji hali inayopelekea  kuvimba.

“Hatari  kubwa ni kuharibu moyo na figo chumvi ikijaa inapata shida.

“Kwa habari ya moyo inaweza kusababisha mshtuko wa moyo na hata  kiharusi kwasababu chumvi imekuwa nyingi ukifanya hivyo kwa muda mrefu.

“Athari nyingine mifupa inakuwa na calcium ambayo mara nyingi ikitaka kutoka inapitia mkojo kama kwenye chakula huna calcium nyingi  mifupa inakuwa laini na inakuwa rahisi kuvunjika,”anaeleza Dk Nkubi.

 MIKAKATI YA  INAYOFANYIKA

Mikakati ya kuzuia upungufu wa madinin joto ulianza kuhusisha matibabu kwa kutumia vidonge ,matone na sindano za madini joto kwa muda mfupi.

Kutokana na mkakati huo kuwa wa gharama kubwa na usioendeleavu  mwaka 1994  uwekaji wa madini joto kwenye chumvi ulianzishwa  kama mkakati endelevu na wakudumu .

Mkakati huo unafanikiwa kutokana na teknolojia ya uchanganyaji chumvi kuwa rahisi  kwani chumvi iliyochanganywa na madini joto haibadiki rangi,harufu wala ladha yake.

Bei ya chumvi ni nafuu sana hivyo wananchi wanaweza kumudu  hivyo chumvi hutumiwa na idadi kubwa ya watu.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo anasema mkakati ambayo inafanyika  ili kuhakikisaha kiwango cha matumizi ya chumvi yenye madini joto toshelevu ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii.

“Pia tunatoa mafunzo kwa  maafisa afya na wazalishaji wa chumvi kuhusu umuhimu wa madini hayo,madhara yatokanayo na upungufu wa madini hayo  na uzalishaji wa chumvi bora yenyewe madini joto na ufuatiliaji wake.

“Tunahamasisha viongozi na kamati za ulinzi na usalama katika ngazi zote  na pia tumeanzisha chama cha wazalishaji chumvi ili kuwaunganisha  na wadau wengi hii itawaezesha kuzalisha chumvi bora yenye madini joto ya kutosha.

“Kingine tunafatilia uzalishaji wa chumvi yenye madini joto ya kutosha  na vifaa vingine  na mkakati mwingine ni kuwepo  kwa kamati ya kitaifa inayoratibu mpango wa kudhibiti upungufu wa madini joto yenye uwakilishi kutoka sekta mbalimbali,”anaeleza Dk Lyena.