December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo:Nimekuja Songwe kufanyakazi

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

MKUU mpya wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, ameanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake mapya kwa kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kwenye nafasi hiyo, huku akisema ameenda Songwe kufanyakazi.

Ametoa kauli hiyo, leo Machi 19, 2024 wakati akizungmza na viongozi na watumishi wa serikali, Taasisi za umma, dini, mila na vyama vya siasa katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Francis Michael ambaye alitenguliwa hivi karibuni.

“Naomba niwashukuru viongozi na watumishi wenzangu wa Mkoa wa Songwe kwa mapokezi mazuri na makubwa mlionifanyia asubuhi ya leo, kwani yamenipa nguvu na ari ya kuja kufanya kazi kwa bidii kubwa kwani nimewakuta wenzangu wakinisubiri tuje kuendeleza gurudumu kwenda mbele,Nimekuja Songwe kufanya kazi,”amesema Chongolo

“Lakini pia nimshukuru kaka yangu Dkt. Francis (Rc aliyetenguliwa) amenikabidhi ofisi muda si mrefu uliopita na nilikuwa napitia taarifa kabla sijafika robo akapata bahati ya kuinuka yeye kwa ajili ya kutoa salamu za kuaga na kunikaribisha kwenye salamu amenirahisishia kuisoma taarifa yote na sasa ipo kichwani , mimi ndiyo nimekabidhiwa na taarifa tumeipokea wote kwa pamoja hapa kuna haja ya kuirudi chochote, itoshe tuu kusema nawashukuru …nimekujaa kufanya kazi” amesema Chongolo.

Chongolo amesema anatarajia kuanza majukumu yake hayo mapya kwa kuwajibikaa kwa nguvu na moyo wake wote, kwani wananchi wa Songwe wanahitaji viongozi waliopewa dhamana kufanya kazi za kuwaletea maendeleo.

Aidha, Chongolo ameongeza kuwa, yeye kama Mkuu wa Mkoa atafanya kazi yake ya uratibu na uongozi ili kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Songwe wanapata maendeleo, hivyo amewataka watendaji waliopo chini yake nao kukaa sawasawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa aliyemaliza muda wake, Dkt. Francis amemuomba Chongolo kushughulikia changamoto kuu zinazoukabili mkoa huo, ambazo ni kasi ya ongezeko la mimba za utotoni ambapo zinafanya Mkoa huo kuwa kinara wa tatizo hilo nchini.

Ametaja changamoto nyingine ambazo ni ubovu wa miundombinu ya barabara, zikiwemo barabara Kuu muhimu kwa uchumi kwa Mkoa wa Songwe, ambazo ni barabara kuu ya Mlowo –Kamsamba yenye urefu wa kilimeta 135 ambayo ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao ya kilimo kama mpunga na ufuta.

Ikiwemo barabara nyingine ya Mbalizi-Mkwajuni hadi Patamela yenye urefu wa kilometa 116 ambayo ni muhimu katika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Uteuzi wa Chongolo Mkoani hapa, unafanya idadi ya wakuu wa mikoa walioongoza mkoa huo tangu kuundwa kwake kufikia sita, ambapo mwaka 2016 Hayati John Magufuli alimteua Chiku Galawa kuwa Mkuu wa mkoa wa kwanza na kufuatiwa na Brigadia generali Nicodemasi Mwangela (2019-2021), Omari Mgumba (2021-2022), Waziri Kindamba (2022-2023) Dkt Francis Charles (2023-2024)na Chongolo ni wa sita.