Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chongolo amesema kuwa imani za kishirikina ni umaskini huku akiwasihi wananchi wa Mkoa wa Katavi kuacha kuwapa nguvu na fursa watu wanaodhaniwa kuwa na uwezo wa kufichua wachawi maarufu kwa jina la Kamchape au lambalamba kwani wanafanya mambo yanayokiuka sheria za nchi.
Chongolo ametoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua ambaye amesema kuwa kitendo hicho kiliweza kuhatarisha amani na usalama wa mkoa hususani katika mwambao wa ziwa Tanganyika.
Chongolo amesema kuwa imani za kishirikina ni umasikini na kama jamii inapaswa kujifunza kwa kuagalia watu wengi wanaoamini katika ushirikina kwani wanaami kwenye ndoto ambazo kutekelezeka kwake ni ngumu.
“Achaneni kuendekeza mambo yanayoweza kutoa taswira ya umasikini kwa Mkoa wetu” amesisitiza.
Amesema kuwa Mkoa wa Katavi ni mkubwa ambao umejenga historia kubwa kwa kuwa na watu wasomi kama Mhadisi Azaki Kamwele ambaye ni mtumishi wa serikali kwa miaka mingi sambamba na Mizengo Pinda Waziri Mkuu Msitaafu,Iddi Kimata Mkuu wa Mkoa Msitaafu na Mkoa wa watu wazito kwenye nchi hii hauwezi hadi leo ukawa unaendekeza ushirikina kama daraja la kufanikiwa kimaisha.
Katibu Mkuu huyo amesema ni lazima Mkoa utoke kwenye kufikiri mambo kwa njia rahisi kwa sababu maendeleo hayapatikani kwa nduba,kupuliza,kupiga lamli na kutengeneza mambo rahisi kwenye mambo yanayohitaji kufuata utaratibu.
“Ukiona watu wa namna hiyo wala usipate shida angalia wanaishi kwa masharti mtu anaweza kuwa na ng’ombe 1000 lakini kwake haruhusiwi kula nyama nusu kilo kwa wiki sababu masharti yanayotolewa na watu wanaopenda kupulizapuliz,achaneni na maisha hayo kwani niafadhari uwe na ng’ombe 10 uwe na uhuru wa kula nyama,” amesema Katibu Mkuu huyo.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa mila potofu zinawatenganisha na zinawatengenezea uadui usiyo na maana, zinawakwamisha kwenye shughuli za maendeleo.
“Akija mtu hapa akapiga kamchape yake akawaambia ukilima shamba hili hutavuna mwaka huu unaacha kwa sababu unaamini alichosema ,je yeye ni Mungu?,yeye ni mvua?,yeye ni ardhi?na yeye ni mbegu?,”amehoji Chongolo ambapo wananchi walijibu kwa kukataa kuwa sio Mungu.
Zuena Rashidi,Mwananchi na mkazi wa mtaa wa Kawajese ameshukuru ujio wa Katibu Mkuu huyo kwani anaamini kuwa utakuwa sehemu ya kusikiliza kero za wananchi na kufanyiwa kazi kwa muda muafaka.
Amesema kuwa CCM ilipewa dhamana ya kuongoza serikali hivyo wanapaswa kuwajibika kwa kutatua kero ambazo zimekuwa kikwazo kwa usitawi wa uchumi.
Jumanne Magaga anasema kuwa Mkoa wa Katavi una changamoto nyingi hususani ya migogoro ya mashamba,mipaka kati ya wananchi na hifadhi mbalimbali zilizopo mkoani Katavi ambapo kama Katibu Mkuu huyo ataweza kuzishughulikia wataweza kuishi kwa amani.
Mwananchi huyo ameeleza kuwa Katibu Mkuu anapaswa kuwaonya watendaji wa serikali ambao wamekuwa kikwazo cha wananchi kwenye kufanikisha maendeleo yao kwa kuwa wabadhirifu na wapenda rushwa.
Katibu Mkuu wa CCM Taifa,Daniel Chongolo yupo kwenye ziara ya siku 5 katika Mkoa wa Katavi ambapo atakangua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo sambamba na kuangalia uhai wa chama hicho.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi