December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo atoa miezi miwili TAMISEMI kupeleka fedha Tanganyika

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi

Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeagizwa ndani ya miezi miwili kuhakikisha inatoa fedha haraka kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kituo cha afya kilichopo wilayani Tanganyika.

Kituo hicho ambacho kinatarajiwa kuwa hospitali teule ya Wilaya ya Tanganyika ili kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kata za Ikola,Karema,Kapalemsenga na Isengule wilayani humo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo akiwahutubia wananchi wa Kata ya Kasekese h
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi

Ujenzi huo unajengwa Kata ya Ikola tarafa ya Karema kwa fedha za mapato ya ndani kwa kuwa eneo hilo ni lango kuu la biashara kati ya Tanzania na nchi ya DRC Congo ikiwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi maeneo hayo ambao kwa sasa hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya km 100 kwenda Makao Mkuu ya wilaya hiyo kwa ajili ya kutafuta huduma ya matibabu katika hospitali ya wilaya.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Daniel Chongolo ametoa agizo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

“Lakini niseme kwa kasi ninayoiona tutachelewa kufikia malengo na Kata ya Ikola haina kituo cha afya, nimeagiza mletewe fedha ya kituo cha afya ili iwaongezee mwendo wa kujenga miundombinu itakayowezesha kufanikiwa lengo la kuwa na hospitali teule,”amesisitiza.

Amesema kuwa ni lazima kuhakikisha miundombinu yote ya kituo cha afya inakamilika kwani TAMISEMI hawawezi kushindwa kwenye vitu vidogo kwa kuleta fedha zitakazo fanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo.

“Nafahamu Waziri wao anakimbia kasi ‘speed’ kubwa sasa moja ya kukimbia ni kuleta fedha kwenye kituo hiki cha afya cha Ikola,idadi ya watu ni kubwa nasisitiza viongozi kusimamia fedha za umma pindi zitakapoletwa,”.

Kuhusu upungufu wa watumishi zaidi ya 200 wa afya aliosema Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijiji Selemani Kakoso Katibu Mkuu wa CCM ameahidi kuichukua changamoto hiyo licha ya serikali kutoa vibali vya kuajiri watumishi wa afya zaidi ya 8000 lakini bado mfumo wa kupeleka watumishi hao maeneo ya mji unaendelea.

Ambapo amesema atawasiliana na TAMISEMI kuhakikisha inatafuta watumishi popote pale walipo na kuweza kufikishwa katika Wilaya ya Tanganyika.

“Kushusha watumishi katika Wilaya ya Tanganyika kutapunguza changamoto ya upungufu wa watumishi hao,hatuwezi kuwa na watumishi sehemu zingine kwa asilimia 80,sehemu zingine 90 na sehemu nyingine 50 ni kutokutimiza wajibu,”.

Awali Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini,Selemani Kakoso amesema kuwa Wilaya ya Tanganyika ilikuwa na vituo vya afya vitatu ambapo kwa sasa kila kata kumejengwa kituo cha afya jambo ambalo anaipongeza serikali kwa kutoa fedha na imewashirikisha wananchi kupitia halmashauri ya wilaya na kijiji kufanikisha ujenzi huo.

Kakoso amesema kuwa lengo la kujenga ilikuwa ni kujianda na mradi mkubwa ambao serikali imewekeza wenye thamani ya zaidi ya bilioni 48 wa bandari ya Karema kwa kutambua kuwa maeneo hayo yatakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Kasekese

Kwa sababu ziwa Tanganyika imepakana na nchi ya DRC Congo,Burundi na Zambia ikiwa eneo hilo ni sehemu ya mji mdogo ambao unakua ambapo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri hiyo waliamua kujenga

Mbunge huyo amesema kuwa baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya alimjibu haiwezi kujenga hospitali mbili kwenye wilaya lakini alimuomba Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo kwa kuwa amejionea umbali wa kijografia uliopo kati ya makao makuu na Tarafa ya Karema hivyo ameomba kiasi cha fedha cha milioni 700 kupatiwa kwa ajili ujenzi wa hospitali hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwamvua Mrindoko amesema kuwa umuhimu wa hospitali teule malengo yake ni kuhakikisha kwamba bandari itakapokuwa imeanza kufanya kazi masuala yote ya kitabibu yaweze kuwa karibu.