Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi.
Wananchi Mkoa wa Katavi wamehakikishiwa upatikanaji wa umeme wa grid ya taifa kwa haraka ambao utachochea ukuaji wa sekta ya viwanda na shughuli zingine za kiuchumi katika Mkoa huo.
Umeme unazalishwa kwa sasa mkoani humo unatokana na mitambo ya genereta zikiwa Megawati 6.25 ambazo huzalishwa katika kituo cha Wilaya ya Mlele na Manispaa ya Mpanda huku mahitaji ya Mkoa ni zaidi ya Megawati 10 hivyo kuwa na upungufu wa zaidi ya Megawati 4.
Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Mpanda katika ofisi ya CCM Mkoa wa Katavi amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatabua changamoto hiyo ambapo itashughulikiwa kwa haraka na kuandika historia ya kuwa na umeme wa uhakika.
Ambapo amesema kuwa atamwita Waziri wa Wizara ya Nishati kuja mkoani Katavi kwa ajili ya kuona uhalisia wa utekelezaji wa mradi na kuhakikisha anaweka nguvu zake zote ili wananchi wa Mkoa huo waweze kupata umeme wa grid ya taifa utakao wawezesha kufungua viwanda mbalimbali vya kuchakata alzeti na mazao mengine.
Chongolo amesema kuwa katika taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko na viongozi wengine wamesisitiza sana kuhusu suala la umeme na ujenzi wa laini ya grid ya taifa kutoka Mkoa wa Tabora hadi Mpanda.
“Sisi tuliahidi mikoa hii yote ambayo ilikuwa haijaunganishwa na grid ya taifa ikiwemo Kigoma,Katavi na Rukwa tutahakikisha inauganishwa kwa kipindi cha miaka 5 ya utekelezaji wa ilani ya CCM,”amesema Chongolo.
Amesema kuwa kwa sasa Mkoa wa Kigoma na Rukwa kwa sehemu kubwa umeshauganishwa na umeme lakini Mkoa wa Katavi bado.
“Matamanio yangu ni kutokuwa na ahadi hewa ambazo zitasubua ili kufikia malengo,nitakwenda kuwaita wanaohusika na mambo haya hususani Waziri anayehukika na hiyo TANESCO na bahati nzuri amepewa mamlaka makubwa hivyo hana sababu ya kujitetea,”amesema Chongolo.
Hivyo anaenda kusukuma mradi huo ili uwe histori kwani hawawezi kuwa na barabara nzuri ya kutoka Tabora mpaka Katavi lakini umeme unaosimamisha nguzo tu ukawashinda.
Aidha katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amesema amekuja mkoani Katavi ili kujionea uhalisia wa utekelezaji wa ilani ya CCM hivyo hatapenda mazungumzo ya kupeana sifa tu bali anahitaji kuelezana matatizo yanayokabili mkoa huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi,Idd Kimata amesema kuwa changamoto ya umeme kama itashughulikiwa kwa wakati mkoani Katavi shughuli nyingi za uzalishaji zitafanikiwa hususani kwenye eneo la viwanda ambapo kwa sasa wanashindwa hata kuita wawekezaji.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi