Na Mwandishi wetu,Timesmajira Online
CHAMA Cha Mapinduzi kimemuagiza mkuu wa mkoa wa Rukwa
Joseph Mkirikiti kuunda kikosi kazi cha kukagua na
kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa mkoani humo
ili kujua ikiwa utekelezaji wake unakidhi thamani ya
fedha zilizotumika.
Kimebainisha kuwa hakikuridhishwa na miradi
walioitembelea hasa katika sekta ya afya ambayo
inayokabiliwa na changamoto kubwa ya dawa, wataalam,
huduma duni kwa wazee pamoja na maeneo mengine kuwa
na utekelezaji wa miradi isiyoendana na thamani ya
fedha iliyotumika
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa chama hicho Ndugu
Daniel Chongolo katika kikao cha majumuisho ya ziara
yake ya siku mbili mkoani humo, iliyoambatana na
wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM
Taifa, kilichofanyika ukumbi wa mikutano manispaa ya
Sumbawanga.
“Naagiza na kukuelekeza mkuu wa mkoa uunde timu ya
wataalam kwa ajili ya kukagua na kufanya tathmini ya
miradi yote inayotekelezwa mkoani kwako ili kujua hali
halisi ya kinachoendelea hususani kwenye eneo la
thamani ya fedha zilizotumika hapa, mambo hayaendi
vizuri kabisa” Amesema Chongolo.
Amefahamisha kuwa CCM haiko tayari kuwalea viongozi na
watendaji wazembe wanaoonekana kushindwa kutatua kero
za wananchi na kuimarisha ustawi wao, hivyo kati siku
14 atahitaji kupata ripoti ya utekelezaji wa maelekezo
hayo na hatua kali zichukuliwe itakapobainika kuna
ubadhirifu ama uzembe ambao unakwambisha ufanisi wa
miradi hiyo.
“Nahimiza watendaji wa serikali kuwa waadilifu kwa
kuheshimu fedha za umma. Hakikisheni fedha zinazoletwa
au kutengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo
zinatafsirika kwa wananchi kwa kuwaletea unafuu na
kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi kwao.”
Amesema Chongolo.
Hata hivyo, Chongolo amesema atakaporejea Dodoma
watawaita mawaziri wanaohusika na sekta za afya, maji,
ardhi na Tamisemi ili kujiridhisha juu ya mipango yao
na kujua mkwamo ama urasimu unatokea katika eneo gani
na kupelekea huduma kusuasua na kuwa sio za kiwango
cha ufanisi kwa wananchi.
“Tunataka watueleze nani anasababisha mkwamo katika
upatikanaji wa huduma, nasema hivi nikitambua sisi
viongozi tunawajibu wa kufuatilia na kusimamia,
tutakuwa wakali, ni lazima tuogope fedha ya umma,
ukizitumia vizuri zitakujengea heshima, ukizitumia
vibaya zitakuvunjia heshima kwa wananchi, hivyo kila
mmoja anapaswa kuwa mwadilifu katika kusimama dhamana
aliyopewa,” Amesema Chongolo
Amesema, kila kiongozi na mtendaji katika chama na
serikali anawajibu wa kutimiza wajibu wake kwa
kuhakikisha upatikanaji wa tija huduma za kijamii
unakuwepo kama anavyosisitiza Rais Samia Suluhu
Hassan wakati wote.
More Stories
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo