Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online. Korogwe
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chongolo amewaonya wanachama wake wasitumie Uchaguzi Mkuu wa chama hicho mwakani, kupanga safu za uongozi kwenye nafasi za Udiwani na Ubunge 2025 na badala yake, watumie nafasi za kuomba uongozi kwa ajili ya kuimarisha chama.
Akizungumza jana nje ya Ofisi ya CCM Shina Namba Mbili, Tawi la Kijiji cha Welei Kata ya Lewa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Chongolo amesema uchaguzi unaofanyika mwakani ni kwa ajili ya kupata viongozi ambao watakisaidia chama kuvuka salama miaka mingine mitano, lakini si uchaguzi kwa ajili ya kupanga safu kwa watu wanaotaka uongozi mwaka 2025.
“Chama Cha Mapinduzi, mwakani tuna Uchaguzi Mkuu. Uchaguzi huo si kwa ajili ya kupanga safu kwa watu wanaotaka uongozi kwa nafasi mbalimbali ikiwemo Udiwani na Ubunge. Uchaguzi huu ni kwa ajili ya kuimarisha chama, waacheni Madiwani na Wabunge wafanye kazi, acheni kupitapita ama kutaka kujenga makundi ya kutaka uongozi.
“Nataka kuwaeleza, viongozi watakaochaguliwa mwakani wawe waadilifu, waaminifu na watakaoweza kukisaidia chama kuendelea kuongoza nchi hii. Na kipimo cha kwanza ni kuchagua viongozi wanaokijua chama, wanaoshirikiana na chama, tunataka kupata viongozi ambao wanashiriki vikao vya chama na msingi wa kwanza wa kiongozi mzuri ni kushiriki vikao vya shina, sababu hakuna kiongozi anayetokana na tawi, kata, wilaya, mkoa au taifa, bali shina,” amesema.
Akijibu hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Shina Namba 2 katika Tawi la Welei Agness Chalema, Chongolo amesema kilio cha wananchi wa Kata ya Lewa kutaka kupata kituo cha afya, atalifikisha kwa Rais, Samia Suluhu Hassan ili waweze kupatiwa sh. milioni 500 ili kuunga mkono juhudi za wananchi, kwani tayari walishaandaa eneo na kumwaga mawe.
Chongolo amesema, pia malalamiko yaliyotolewa kuhusu barabara ya kutoka Njiapanda ya Lewa iliyopo Mtaa wa Msambiazi hadi Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Lutindi kilomita 17 ambayo inapita Kata ya Lewa ni mbovu, tayari Rais Samia ametoa sh. milioni 500 kwa kila jimbo ili kuweza kufanya matengenezo ya mara kwa mara kwenye maeneo yao.
Akiwa Shina Namba Moja Tawi la Kiloza Kata ya Magila-Gereza, Chongolo ameitaka serikali kushughulikia suala la vijana wa bajaj na bodaboda, kuona wanapatiwa mafunzo ya udereva ili waweze kuruhusiwa kuendesha vyombo vyao kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Arusha. Ni baada ya Diwani wa Kata ya Magila-Gereza, Mwajuma Kitumpa kulalamika kuwa bajaj zinakatazwa kutembea njia kuu kwa zaidi ya kilomita kumi kutoka mjini Korogwe sababu ya usalama.
Kitumpa amesema wagonjwa na akinamama wajawazito, wanashindwa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Korogwe iliyopo Kijiji cha Makuyuni kwa wakati, sababu inabidi wasubiri mabasi madogo (Coaster) kutoka Tanga ambapo wakati mwingine wanakataliwa kupanda sababu wanakwenda karibu.
Amesema kutoka Kata ya Magila-Gereza hadi Hospitali ya Wilaya ni kilomita nne. Hivyo kama bajaj zingeruhusiwa kusafirisha abiria kutoka Korogwe mjini hadi hospitali takribani kilomita 15, ingewasaidia wagonjwa.
Naye Diwani wa Kata ya Lewa, Yohana Shekwavi amesema wanaomba barabara ya Njiapanda ya Lewa hadi Lutindi kilomita 17 iwekwe lami, sababu njia hiyo ndiyo inakwenda Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Lutindi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava amesema wananchi wameonesha jitihada za kutaka kujengwa Kituo cha Afya Welei na yeye ameunga mkono kwa kupeleka tripu tatu za mawe. pia umeme wa REA umefika kwenye Kijiji cha Welei, lakini bado vitongoji havijapata umeme lakini anaamini umeme utafika kwenye vitongoji vyote.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi