December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chiro amezitaka taasisi kupanda miti na kutunza mazingira

Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Ilala

NAIBU WAZIRI wa Muungano na Mazingira, Hamis Hamza Chiro, amezitaka taasisi za serikali na binafsi kupanda miti kwa ajili ya kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Chiro,amesema hayo jimboni Segerea katika tamasha la Samia ,Nishati Safi “Samia Nishati Safi Festival” lililoandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Janeth Masaburi.

“Naziagiza taasisi binafsi na za serikali zikiwemo za mazingira muanze kampeni endelevu ya kupanda miti ili Tanzania iwe ya kijani,tusiharibu vyanzo vya maji na uchafuzi wa mazingira,”amesema Chiro.

Pia amewataka Watanzania katika kusherekea siku zao za kuzaliwa na kuoa waweke kumbukumbu ya kupanda miti ya vivuli na matunda iwe sehemu ya utaratibu kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji.

Pamoja na Watanzania kuipenda nchi yao na kutumia nishati safi ya kupikia katika juhudi za kuunga mkono Serikali katika kampeni ya Dkt.Samia Suluhu Hassan kila mmoja atumie gesi na nishati mbadala.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Mbunge wa Viti Maalum Wanawake mkoa Dar es Salaam Janeth Masaburi, amekuwa akisemea vizuri kampeni hiyo ya utunzaji mazingira na kutumia nishati safi ya kupikia salama ya gesi pamoja na kutoa elimu kwa mama na baba lishe .

Sanjari na hayo amewahimiza Watanzania kupanda miti katika maeneo yao kwa ajili ya kuinusuru nchi isikumbwe na jangwa kwani kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakikata miti kwa ajili ya mifugo na utengezaji wa mkaa huku akiwataka kubuni nishati mpya.

Akizungumzia changamoto ya mazingira aliwataka wamiliki wa viwanda,migodi na machimbo wasiharibu mazingira badala yake wametakiwa kulinda mazingira na kutunza vyanzo vya maji.