Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
SERIKALI ya China imeahidi kuendelea kujenga na kukuza uhusiano na Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati yenye ubora kwa weledi na uaminifu mkubwa ili kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Ofisa Takwimu wa China,miaka 10 iliyopita kiwango na ubora wa kibiashara na uwekezaji kati ya China na Tanzania kiliongezeka hadi kufikia asilimia 236 sawa na Dola za Marekani bilioni 8.31,mwaka 2022 ambao mwaka 2012 ilikuwa ni Dola za Marekani bilioni 2.47.
Balozi wa China nchini hapa,Chen Mingjian kwa niaba ya Rais wa taifa hilo,Xi Jingping, ameeleza hayo kwa nyakati tofuti mkoani Mwanza, baada ya kukagua ujenzi wa Daraja la JP.Magufuli na Reli ya Kisasa ya Kimataifa (SGR)katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kumi ya kuanzishwa kwa ukanda wa miradi ya barabara (BRI) Tanzania.
Amesema China itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kindugu na Tanzania kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa miundombinu, uwekezaji, masoko na biashara ili kufungua fursa za uchumi kwa Watanzania,hatua itakayoharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Pia,amesema Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo yaliyowezeshwa na kuwepo kwa miundombinu bora na imara iliyotekelezwa kwa weledi na kwa teknolojia ya kisasa.
“Tanzania imekuwa na matokeo chanya (mazuri) na China imekuwa mshirika mkubwa wa kibiashara na chanzo kikubwa cha uwekezaji wa kigeni,viwango na ubora wa biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi umefikia dola za Marekani bilioni 8.31 sawa na asilimia 236,”amesema Mingjian.
Amesistiza kuwa nchi hiyo itaendelea kufanya jitihada zisizo koma kukuza urafiki kati ya China na Tanzania, kuinua ushirika na ushirikiano kuwa wenye tija na manufaa huku miradi wanayoitekeleza ikiwa daraja la kuimarisha urafiki kati ya wananchi wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.
Balozi huyo wa China nchini amesema Tanzania imekuwa karibu zaidi kadiri ya muda unavyokwenda ambapo Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ni kumbukumbu ya milele ya uhusiano huo wa kihistoria kati ya China na Afrika na kuahidi nafasi za masomo nchini humo kwa Watanzania 2000.
“Tanzania kwa miaka mingi inadumisha uimara wa maendeleo mapya yaliyopatikana ya kiuchumi na kijamii,ni yenye ushawishi Afrika Mashariki na Kusini,tunahitaji uaminifu,matokeo ya kweli,uhusiano wenye malengo ya pamoja katika kutafuta maslahi mazuri yenye manufaa kwa wote,”amesema.
Mingjian amesema Tanzania ina mazao na bidhaa nyingi za kilimo, kuna fursa za uwekezaji wa madini yakiwemo ya Tanzanite na imeanzisha safari za anga nchini China.
Mwakilishi wa Wabunge Marafiki Tanzania Geofrey Mwambe,akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wabunge marafiki nchini,amesema ushirikiano wa Tanzania na China ni wa muda mrefu ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K.Nyerere na Mwenyekiti Mao Tse Tung wa China ambapo wabunge hao wamekuja kuangalia miradi ya kukuza uhusiano wa nchini hizo .
“Tanzania na China zimekuwa nchi ndugu (kaka na dada) kihistoria,Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) imejengwa na China miaka 50,imewekeza kwa kiwango kikubwa ikiwemo biashara kwa kuuza bidhaa zake nchini huku kampuni zake 77 zikifanya kazi ya kujenga miundombinu,”amesema.
Kwamba uhusiano huo umeendelezwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, umewezesha wananchi wa pande zote mbili kunufaika kibiashara na uwekezaji huku kukiwa na wataalamu 1200 wa China wakifanya kazi za ujenzi wa miundombinu ambapo kampuni za Bima zimeridhia kampuni zaidi ya 70 kufanya kazi nchini kwa ufanisi.
Mwambe ameeleza wabunge hao wameonesha Tanzania na China ni marafiki wa muda mrefu,dhamira kubwa ni kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kiuchumi,biashara na uwekezaji ili kuleta maendeleo,kutambua na kuenzi mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere na Mwenyekiti Mao.
“Tunapongeza kazi hiyo ya daraja la JPM ni ndoto inakwenda kutimia,linakwenda kufungua uchumi wa Tanzania na nchi jirani ,kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara,Rais Dk.Samia ameshasema hakuna mradi utalala tukishirikiana na China,wanaendelea kuhakikisha miundombinu yetu inaimarika ambapo SGR ni mradi wa kipaumbele cha maendeleo,”amesema.
Mwambe amesema China imewekeza kwa kiwango kikubwa,makampuni zaidi ya 70 yanafanya kazi nchini ikiwemo CCECC,kupitia miradi hiyo wahandisi 200 wa ndani watapata uzoefu na kujifunza teknolojia mpya ya kujenga miundombinu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa Masasi (CCM) umeanzishwa mfumo mpya wa kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa fedha za ndani na wafadhili ambapo mkandarasi atafanya kazi kisha analipwa gharama zake.
Awali Meneja Mkuu wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Afrika Mashariki Zhang Junle amesema ujenzi wa daraja la JPM linaloigharimu serikali zaidi ya sh.bilioni 700 umefikia asilimia 78,huku ujenzi wa reli ya SGR kipande cha tano Mwanza-Isaka,ukigharimu zaidi ya sh.trilioni 3 za Tanzania.
Ameeleza kwa miaka 50 amekuwa wakifanya kazi nchini kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na China,wamejenga miradi mikubwa ukiwemo wa Daraja la JPM , refu Afrika ya Mashariki na la Sita kwa urefu barani Afrika, likipita juu ya maji ya Ziwa Victoria.
Junle alisema daraja hilo linalojengwa kwa teknolojia ya kisasa, litaondoa changamoto ya usafiri,litapunguza muda wa wasafiri na magari kuvuka kwa pantoni kutoka nusu saa hadi dakika tano kutoka Kigongo hadi Busisi.
Balozi Mingjian na wabunge hao marafiki wa China,walikagua miradi ya ujenzi wa Daraja la JP.Magufuli na Reli ya Kisasa ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) ikiwa ni maadhimisho ya kumbukumbu ya kumi ya kuanzishwa ukanda wa miradi ya barabara (BRI) Tanzania ambapo yalishirikisha kikundi cha wabunge marafiki wa Tanzania.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya