March 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Child support Tanzania yapongezwa kutetea maslahi watoto wenye ulemavu

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

SERIKALI mkoani Mbeya imelipongeza shirika la Child support Tanzania  kwa  kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha linatetea maslahi ya wanafunzi wenye ulemavu na kwamba kama mkoa wanajivunia kufanya kazi kwa ukaribu na shirika hilo katika utekelezaji wa mpango mkakati wa elimu jumuishi

Akizungumza Machi 24 ,2025 wakati wa kikao cha matokeo ya tathimin sekta ya elimu kuhusu elimu Jumuishi, Mtaaluma ngazi ya mkoa ambaye alimwakilisha Katibu Tawala mkoa wa Mbeya,Mwalimu Ally Simba amesema kuwa mfumo wa sera na elimu jumuishi kuna kila sababu ya kutilia mkazo ili kuhakikisha inakwenda Sambamba kama walivyo wanafunzi wengine.

“Niseme kwamba nimefarijika sana kuona kikao hiki kikiendelea katika kutetea maslahi ya wanafunzi wenye ulemavu hususani kwa hawa wenzetu Child support Tanzania,kwani wamekuwa mstari wa mbele kutetea masuala ya wanafunzi hawa wenye ulemavu,Mimi binafsi naweza kutoa historia kidogo wakati nakuja mkoa wa Mbeya niliwahi kukaimu nafasi ya elimu Maalum hivyo nilifanya kazi kwa ukaribu na mkurugenzi mtendaji wa shirika la child support na kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri “amesema Mwalimu Simba.

Aidha Mwalimu Simba amesema amesikiliza baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa elimu jumuishi kuwa ni uelewa baadhi ya wadau na walimu katika kutekeleza majukumu bado uelewa ni Mdogo katika kutekeleza kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na ikiwa ni ajenda itasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum wanatafutwa na kupatikana kwa asilimia 100 kwa kushirikisha wadau.

“Tukiongeza kutoa elimu kwa wadau mbalimbali mwisho wa siku tutakua tumesaidia kulisukuma gurudumu hili  nafikiri viongozi wenzangu ngazi ya elimu mtakua mnafahamu kuwa inapofika kipindi cha uandikishaji huwa tunapambana sana kutoa elimu ili kuhakikisha kuwa tunawapata watoto hawa wenye ulemavu ili waweze kuandikishwa shule “amesema

Aidha Mwalimu Simba amesema bado kuna wazazi na jamii ambao wana mfumo wa kuwaficha watoto wenye ulemavu lakini kupitia elimu na mikakati inayowekwa kama wadau wa elimu huwa inasaidia kupatikana   kwa watoto hao na kuingia kwenye mfumo wa elimu .

Akizungumza katika kikao hicho ambacho kimewajumuisha Maafisa elimu kutoka halmashauri mbili pamoja na waandishi wa habari, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Child support Tanzania (CST) Noela Msuya amesema wamekutana kufanya kikao cha kuangalia matokeo ya tathimini waliyofanya sekta ya elimu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa elimu jumuishi.

Msuya amesema kuwa kikao cha Kwanza walifanya mwezi Machi mwaka huu ambapo waliangalia taarifa kutokana na tathimin waliyofanya na kuzileta kwa wadau wa elimu kuangalia kama zipo sahihi.

“Leo tunawasilisha matokeo tuliyopata kwa kwa ngazi juu za uongozi wa elimu  kwa mkoa wa Mbeya kwa hiyo tuna uongozi wa elimu,maafisa elimu, maafisa elimu elimu Maalum,wathibiti ubora wa Shule,wakurugenzi wa Jiji la Mbeya na halmashauri ya Wilaya lengo kubwa kuhakikisha tunaangalia hichi tulichopata katika mpango mkakati wetu wa elimu jumuishi tunaanzia wapi kwenda mbele ili tuweze kutekeleza kwa ubora unaohitajika,mradi huu unatekelezwa na Child support Tanzania kwa kushirikiana na Haki Elimu mradi unaitwa sauti zetu kwa kutekelezwa nchi nzima”amesema mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake,Afisa Uthibiti ubora wa Shule Jiji la Mbeya,Aldo Masonda amesema kuwa mashirika yanayosaidia serikali kuangalia mbinu wanayotumia katika kuwatambua watoto wenye mahitaji maalum na kusema wao wana mbinu nyingi kuliko serikali na kusema serikali ina mzigo  mkubwa na bado kuna  ushahidi wa watoto wengi wanachachwa mtaani na kuona ni kitu cha kawaida tu .