April 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chikota ashauri uwepo wa Sheria ya ugatuaji madaraka

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MBUNGE wa Nanyamba Abdallah Chikota ameishauri Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha Nchi inakuwa na Sera na Sheria ya ugatuaji wa madaraka itakayoweka mipaka ya kiutendaji na hivyo kuondoa sintifahamu za kiutumishi

Akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)mesema uwepo wa Sheria ya ugatuaji wa madaraka itaonesha ni kitu gani kinatakiwa kufanywa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kitu gani kifanywe na Serikali Kuu.

“Kwa miaka mingi sasa tunaongelea Sheria ya ugatuaji madaraka lakini haipo na Sera inayotumika ni ya 1998,hii inakuwa ni vigumu sana katika utekelezaji wa Sera bila sheria,ndiyo maana utakuta leo anakuja kiongozi huyu anasema watumishi sekta ya Afya waende wizarani,kesho anakuja mwingine anasema watumishi Wizara ya Ardhi waende Wizarani mwingine atakuja atasema watumishi Elimu waende Wizara ya Elimu ,

“Lazima tuwe na Sheria ya ugatuaji ambayo itaweka.mipaka ya kiutendaji baina ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu.”

Pia Sheria itafanya kuwepo kwa vyanzo vya mapato vya kuaminika huku akisema vyanzo vilivyopo sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa haviaminiki.

“Kwa hiyo lazima tuwe na Sheria hiyo ambayo itaweka mipaka,vyanzo vya mapato vya uhakika,na vitu gani vitafanywa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu,na hii haitabadilikabadilika kwa sababu itakuwa kwenye Sheria.”amesisitiza

Katika hatua nyingine ameishauri Serikali kuona umuhimu wa kuondoa chaguzi za Naibu Meya na Makamu wenyeviti wa Halmashauri zinazofanyika Kila mwaka na wakati mwingine kusababisha migogoro isiyi ya lazima.

Pia ameishauri Serikali kuangalia muundo wa Kamati za Madiwani lakini pia kuona umuhimu wa kuongeza siku za vikao vya Baraza la Madiwani i Ili kuboresha utendaji wa mabaraza ya Madiwani .

Katika hatua nyingine ameiomba Serikali kupeleka fedha katika Mikoa ya Pwani,Lindi na Mtwara kwa ajili ya kuitengeneza barabara inayopita katika mikoa hiyo ambayo imeathiriwa na kimbunga Hidaya kilichotokea mwaka jana.

“Tarura inafanya kazi nzuri ya kutatua changamoto katika maeneo mbalimbali nchini ,lakini nakuomba mheshimiwa Waziri na timu yako kwamba ,Mikoa hii mitatu ya Pwani,Mtwara na Lindi ni Mikoa iliyoathiriwa na kimbunga Hidaya mwaka jana,barabara ya Kibiti-Lindi pale Somanga na hata barabara za ndani katika maeneo haya zimearhiriwa pia.”amesema Chikota na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo nyongeza ya Fedha ya TARURA iangalie na kupeleka fedha maeneo hayo ili ikatatue changamoto ya barabara hizo na ziweze kupitia wakati wote.”

Amesema barabara zote za ndani katika mikoa hiyo zimeharibiwa na kimbunga hicho huku akiomba fedha zilizoongezwa kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini kipaumbele kiwe katika marekebisho ya barabara hizo.

Kuhusu sekta ya Afya na Elimu Chikota amesema,miundombinu mingi imejengwa lakini Kuna changamoto ya watumishi hasa Mikoa ya pembezoni huku akiishauri Serikali ifanye jitihada za makusudi kutoa kibali Maalum Cha ajira kwa ajili ya Mikoa hiyo ya pembezoni.

Akitolea mfano mkoa wa Mtwara,Mbunge huyo amesema ,mahitaji ya watumishi sekta ya Afya ni 7,309 waliopo ni asilimia 37 tu ya mahitaji huku upande wa Elimu Kuna upungufu wa watumishi wa asilimia 41.

“Kwa hiyo kazi zote tulizofanya kwa sekta ya Elimu na Afya utaona changamoto hazionekani kwa ukubwa wake kwa sababu tunayo miundombinu ya shule ,Vituo vya Afya na Hospitali za wilaya lakini Kuna changamoto kubwa ya watumishi,

“Mfano katika Jimbo langu la Nanyamba tuna X-RAY 2 lakini hatuna mtumishi wa kuendesha hizo mashine ,kipindi Cha nyuma tulikuwa tunaazima mtaalam Kutoka Tandahimba lakini sasa mtaalam huyo amehamishwa “