Na Fresha Kinasa, Times Majira Online,Mara
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, dkt. Pius Chaya , amesema serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuhakikisha uwekezaji unachangia kikamilifu ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.
Dkt. Chaya aliyasema hayo Januari 8, 2026, akiwa katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara, alipofanya ziara ya kukagua na kutembelea maeneo ya uwekezaji, ikiwemo viwanda ambavyo havifanyi kazi katika manispaa hiyo.
Amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana shauku ya kuona uwekezaji unaendelea kukuza uchumi na kusaidia kutatua changamoto ya ajira, hususan kwa vijana wanaohitimu masomo katika vyuo mbalimbali nchini. Kutokana na hilo, alisisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya uwekezaji, kuunganisha nguvu katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, pamoja na kuyawezesha mashirika ya umma kushiriki kikamilifu katika uwekezaji.

“Mwelekeo wa serikali ni kuona uwekezaji wenye tija. Hata hivyo, ni lazima tubadili mitazamo yetu ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa mtazamo chanya. Tumejipanga kuhakikisha mwekezaji akipewa eneo, anaweka wazi dhamira na muda wa kuanza uwekezaji. Lengo ni kukuza uchumi na kuchochea kasi ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Dkt. Chaya.
Akizungumza kuhusu miradi mahususi, Dkt. Chaya alisema Shirika la Reli Tanzania (TRC) tayari limempata mwekezaji wa kujenga Musoma Hotel, na amemuagiza Msajili wa Hazina, anayesimamia zaidi ya mashirika ya umma 300, kukamilisha haraka taratibu zote ili mwekezaji huyo aanze ujenzi mwezi Juni 2026.
Aidha, ameongeza kuwa Mkoa wa Mara una fursa kubwa za uwekezaji kutokana na jiografia yake, ikiwemo kupakana na nchi jirani pamoja na kuwa na Ziwa Victoria lenye fukwe nzuri zinazofaa kwa uwekezaji na utalii. Amesisitiza kuwa serikali imejipanga kuona viwanda vinafufuliwa na kufanya kazi, hatua itakayochochea maendeleo kwa Watanzania.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Benedictor Magiri, alisema Manispaa ya Musoma ilikuwa na kiwanda cha nguo cha Mutex, ambacho kiliwahi kuajiri takribani watu 500 na kuwa tegemeo kubwa la uchumi wa wananchi. Hata hivyo, kiwanda hicho kimekuwa hakifanyi kazi kwa zaidi ya miaka 30, hali iliyozorotesha uchumi wa eneo hilo.

“Kikifufuliwa kiwanda cha Mutex, kitaongeza chachu ya uchumi wa Musoma. Pia kulikuwa na Musoma Hotel yenye eneo kubwa na vyumba karibu 100, lakini kutokana na kukosa mwekezaji, hoteli hiyo imekufa,” amesema Magiri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka, amesema ujenzi na uendeshaji wa Musoma Hotel utachochea kwa kiasi kikubwa utalii wa fukwe za Ziwa Victoria, jambo litakalosaidia kukuza uchumi na kuwaletea maendeleo wananchi wa Musoma kwa ujumla.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi