Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI), Abdallah Chaurembo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutafuta fedha kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Chaurembo amesema hayo alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kamati yake iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Pia Chaurembo amesema, Kamati yake inamshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha ambazo zimetekeleza Mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Mtaa wa Wikichi ambao umesogeza karibu huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Mbali na hayo Chaurembo ameongeza kuwa, Kamati yake imepokea taarifa kutoka kwa Mratibu wa TASAF wa eneo hilo pamoja na kukagua zahanati hiyo iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 89 iliyojumuisha na vifaa tiba, hivyo imeridhika kutokana na kazi nzuri iliyofanyika.
Vilevile, Chaurembo amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Ladislaus Mwamanga kwa kupeleka wataalam ambao wamesimia vizuri ujenzi wa zahanati hiyo.
Aidha Chaurembo amempongeza pia mratibu wa TASAF kwa kusimamia vema fedha zilizotolewa na Mhe Rais kujenga Zahanati hiyo ambayo imekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.Sanjari na hilo, Mhe. Chaurembo amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Wikichi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kuhakikisha ujenzi wa Zahanati hiyo unakamilika kwa wakati.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) inaendelea na ziara yake ya kikazi kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) katika Halmshauri ya Wilaya Mji Njombe.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote