Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
MBUNGE wa kuteuliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda, amempongeza Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, akisema uteuzi huo ni uthibitisho wa uadilifu na uwezo wake mkubwa katika usimamizi wa masuala ya kiuchumi na fedha za umma.
Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa na wabunge kwa Dkt. Nchemba, Chatanda alisema kuwa tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, miradi mingi ya kimkakati na maendeleo nchini imefanikiwa kutokana na uwezo wake wa kusimamia fedha na kuhakikisha upatikanaji wa mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Baada ya kuwa Waziri wa Fedha, miradi yote iliyotekelezwa nchini imefanikiwa kutokana na usimamizi wake makini wa fedha na jitihada zake za kuongeza mapato kupitia TRA. Ndiyo maana tumeweza kushuhudia miradi mikubwa ikitekelezwa katika kila wilaya,” alisema Chatanda.
Akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua Dkt. Nchemba, Chatanda alisema,
“Hakika Rais ametuletea mtu bora ambaye atatusimamia na kuhakikisha tunasonga vizuri katika utekelezaji wa Ilani ya CCM.”
Akizungumzia kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa, Chatanda alisema kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu kumekuwa na ongezeko kubwa la wanawake waliogombea na kushinda majimbo mbalimbali.
“Safari hii tulihamasisha sana wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, na matokeo yake wanawake wamejitokeza kwa wingi na kushinda majimbo karibu 37. Pia kwenye viti maalum wanawake 114 wamepata nafasi. Wanawake hawa wanatarajiwa kuwasilisha changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini,” alieleza.
Ameongeza kuwa wanawake wanatarajia kupewa kipaumbele katika uwezeshaji wa kiuchumi, hasa kupitia asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri zinazotengwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.
“Tunatarajia viongozi wetu watahakikisha fedha hizo zinapatikana kama inavyopangwa, na pia zile shilingi bilioni 200 ambazo Rais aliahidi kwa ajili ya uwezeshaji wa wafanyabiashara wadogo wadogo zitawafikia walengwa. Tunakusudia kuwahamasisha wanawake wengi zaidi kunufaika na mikopo hiyo katika siku 100 za mwanzo kama alivyosema Rais,” alisisitiza Chatanda.
Kwa ujumla, Chatanda alisema ana imani kuwa chini ya uongozi wa Dkt. Mwigulu Nchemba kama Waziri Mkuu, Tanzania itaendelea kusonga mbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwawezesha wananchi kiuchumi, hasa wanawake.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama