Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chata, amesema atahakikisha anatekeleza majukumu yake ya kibunge kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, pamoja na kutetea masuala yanayohusu wanawake nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Bungeni jijini Dodoma Leo Nov 11,2025, Bi. Chatanda alisema kipaumbele chake kikubwa kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo, kwa sababu ndicho walichoahidi wananchi wakati wa kampeni.
“Kama mbunge mteule wa Viti Maalum, nipo tayari kuisimamia utekelezaji wa Ilani ya chama chetu ambayo tuliinadi kwa wananchi. Tutahakikisha Ilani hiyo inatekelezwa kwa sababu tumeshawaahidi wananchi, hususan wanawake, kwamba tutakuwa tukikutana nao mara kwa mara kusikiliza kero na changamoto zao,” alisema.
Chatanda alitaja miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanawake nchini kuwa ni ukatili wa kijinsia na ukatili wa watoto , ukosefu wa mitaji ya biashara na changamoto katika upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
“Tutahakikisha wanawake wanapata mikopo ya asilimia 10 kwa wakati, lakini zaidi tutasimamia utoaji wa elimu na mafunzo ili wanawake hao waweze kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa. Wanawake wakipewa elimu watatambua umuhimu wa kuzalisha, kupata faida, na kurejesha mikopo hiyo ili wanawake wengine pia wanufaike,” alisisitiza.
Aidha, aliipongeza serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupata kura za kishindo asilimia 97.6 katika uchaguzi wa hivi karibuni, akisema hiyo ni ishara ya imani kubwa ambayo wananchi wanayo kwake kutokana na kazi kubwa alizozifanya ndani ya miaka minne.
“Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hii ni imani kubwa ambayo wananchi wamempa kutokana na uongozi wake makini na utekelezaji wa ahadi zake. UWT kwa niaba ya wanawake wote tunampongeza na kumuunga mkono kwa dhati,” alisema.
Chatanda alimalizia kwa kusema kuwa kama Mwenyekiti wa UWT Taifa na Mbunge wa Viti Maalum, ataendelea kushirikiana na wanawake katika ngazi zote za jamii kuhakikisha wanapata fursa za kiuchumi na kijamii ili kujikwamua kimaendeleo.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina