January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chanjo ya Polio kwa watoto ni ya muhimu siyo ya kupuuzwa

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online

MOJA ya magonjwa hatari ya kuambukiza hapa nchini ni ugonjwa wa kupooza viungo vya mwili, maarufu kwa jina la “Polio” na mpaka hivi sasa ugonjwa huu inasemekana haujapatiwa tiba hivyo ili kuuepuka ni kujikinga kwa kupata chanjo.

Mara nyingi mlipuko wa ugonjwa huu hutokea zaidi vipindi vya kiangazi ambapo mtu ye yote anaweza kuathiriwa japokuwa watoto wenye umri wa kuanzia umri wa 00 hadi miaka mitano huwa katika hatari zaidi ya kuambukizwa.

Kiuhalisia Polio ni moja ya virusi ambavyo ndivyo vikimpata binadamu husambaa kwenye mfumo wa neva na hivyo kuweza kusababisha udhaifu wa misuli ya miguu, mikono, mgongo na shingo.

Hali ya namna hiyo inapomtokea mtu husababisha matatizo ya kutembea na kufanya shughuli za kawaida, hata kupumua na baada ya muda husababisha viungo kubana, misuli kunywea au hata kupooza. Dalili huweza kujirudi miaka baada ya maambukizi ya awali.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, dalili za awali za maambukizi ya polio ni mtu kuwa na mafua ikijumuisha na homa, maumivu katika koo, kutapika na maumivu ya kichwa.

Inaelezwa kuwa ugonjwa huu husambazwa kwa mtu kugusana na mtu aliyeambukizwa, kinyesi au kamasi zenye maambukizi ambapo tangu miaka mingi iliyopita mataifa mengi yamekuwa yakiendesha kampeni za kujikinga na gonjwa hili hatari.

Pamoja na kwamba polio huweza kumpata mtu ye yote lakini bado kama nilivyosema hapo awali watoto chini ya umri wa miaka mitano ndiyo walioko kwenye hatari zaidi hivyo nchi nyingi zimekuwa zikiweka mkazo zaidi kwa watoto kupatiwa chanjo ya kinga ya polio.

Kama inavyoelezwa kila wakati polio mpaka hivi sasa haina tiba bali matibabu yanayotolewa mara nyingi hulenga kupunguza dalili za ugonjwa kwa mgonjwa kupatiwa dawa za maumivu kwa lengo la kupunguza  maumivu ya kichwa na misuli.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa hapa duniani ambayo yamekuwa makini sana katika kuhakikisha chanjo ya polio inatolewa kwa watoto kwa kuzingatia muda wa utolewaji wake ambapo kwa mwaka huu wa 2022 kuanzia Desemba mosi hadi Desemba nne chanjo hiyo itatolewa kwa watoto nchi nzima.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Waziri wa Afya hapa nchini, Ummy Mwalimu alinukuliwa akisema katika awamu ya tatu ya chanjo iliyofanyika kuanzia Septemba 01 – 04 mwaka huu watoto wapatao 14,690,597 wenye umri chini ya miaka mitano upande wa Tanzania Bara walichanjwa.

Ilielezwa kuwa kutokana na uhamasishaji mkubwa unaofanyika katika mikoa mingi hapa nchini kuhusiana na utolewaji wa chanjo hiyo kwa watoto, Tanzania iliweza kuvuka lengo lililokuwa limekusudiwa la kuchanja watoto 12,386,854 ambapo hata hivyo waliochanjwa walikuwa ni watoto 14,690,597 sawa na asilimia 118.6 ya lengo.

Kampeni hii ya chanjo inayoendelea hivi sasa nchini kote imetokana na taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo mnamo Februari, 2022 lilitangaza kuwepo kwa mlipuko wa virusi vya polio kule nchini Malawi ambako wagonjwa wawili waliripotiwa ambapo pia visa vinne vya maambukizi ya ugonjwa huo viliripotiwa nchini Msumbiji.

Mwaka 2015 nchi ya Tanzania ilithibitishwa kutokuwepo kwa ugonjwa wa polio ambapo pia tangu mwaka 1996 hapajagunduliwa kisa chochote cha polio hali ambayo inabidi kila mtanzania kuhakikisha anachukua tahadhari ya kutotokea tena kwa ugonjwa huo kwa kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo ya kujikinga na polio.

Mkoa wa Shinyanga ni moja mikoa hapa nchini inayotajwa kufanya vizuri katika utoaji wa chanjo ya polio ambapo kwa awamu zote tatu za utolewaji wa chanjo hiyo imekuwa ikivuka lengo ambalo huwa imejiwekea.

Baadhi ya wazazi mkoani humo wametoa shukrani zao kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kuhakikisha chanjo ya polio inatolewa kila pale inapoonekana haja ya kufanya hivyo kwa lengo la kuwaweka salama watoto wa kitanzania.

Salma Masoud, Agatha Elias na Masumbuko Charles wakazi Manispaa ya Shinyanga wanasema ugonjwa wa polio ni miongoni magonjwa hatarishi hasa kwa watoto na mtu asipozingatia anaweza kujikuta mtoto anapata ulemavu wa viungo vyake vya mwili.

“Binafsi mara zote Serikali inapotangaza kutolewa kwa chanjo hii, huwa nahakikisha watoto wangu nawapeleka kituoni ili waweze kuchanjwa, na awamu hii ninashukuru utaratibu uliowekwa kwa vile watoa huduma watapita majumbani, ni jambo jema, niwaombe wazazi wenzangu tutoe ushirikiano kwa kuhakikisha watoto wetu wanachanjwa,” anaeleza Salma.

Katika awamu hii ya nne inayoanza Desemba mosi hadi Desemba 04, 2022 mkoa wa Shinyanga unatarajia kutoa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wapatao 521,025 ambapo tayari dozi zipatazo 614,800 zimeishapokelewa.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Faustine Mlyutu amesema utaratibu wa utolewaji wa chanjo hiyo kwa awamu hii ya nne utakuwa ni wa nyumba hadi nyumba hali ambayo itawezesha kuwafikia walengwa wengi.

Mlyutu anasema, “…Ni jambo la faraja kwetu na mkoa kwa ujumla kuona wakazi wetu wa mkoa huu kwa sasa wameelewa umuhimu wa hii chanjo ya polio, kupitia kampeni na maandalizi tunayoyafanya tumekuwa na mafanikio makubwa sana,”

“Tangu tuanze kutoa hizi chanjo huwa tunaweka asilimia mia moja, lakini awamu ya kwanza hadi ya tatu mkoa wetu tumefanikiwa kuvuka lengo zaidi ya asilimia mia moja, tunaomba wanahabari tusaidiane katika kufikisha ujumbe kwa wananchi ili na awamu hii ya nne tuvuke lengo pia.”

Hata Dkt. Mlyutu ametoa wito kwa wananchi wa Shinyanga wawe tayari kuwa majumbani wakati wa kampeni hii ya awamu ya nne ili wahudumu wa afya waweze kuwakuta na kuwapatia chanjo watoto wao.

Mratibu wa chanjo katika mkoa wa Shinyanga, Timothy Sosoma anasema mafanikio yaliyopatikana yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushiriki mkubwa wa viongozi wa Serikali, kisiasa na Taasisi za kidini na wadau wengine mbalimbali na kujitoa kwa watoa huduma za afya katika kufanikisha utekelezaji wa kampeni.

“Katika awamu hii ya nne tumejipanga kuongeza timu za uchanjaji na kuwaelekeza wazazi kuhakikisha kwa wale wanaokwenda makazini, basi waache watu wa kuwaangalia watoto ili waweze kupatiwa chanjo pale watoa huduma watakapofika kwenye makazi yao,”

“Timu zitakazofanya kazi katika kampeni hii ni 1,021 ambao miongoni mwao wamo wachanjaji, watunza takwimu na wahamasishaji.  Tayari tumepokea jumla ya chanjo dozi 614,800 pamoja na vifaa vingine (Mark pen, Chaki, Vipeperushi na Rejista,” anaeleza Sosoma.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akimpatia chanjo mmoja wa watoto wa Manispaa ya  Shinyanga katika uzinduzi wa chanjo ya awamu ya nne mkoani Shinyanga.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Faustine Mlyutu akifafanua jambo kuhusu utolewaji wa chanjo ya polio awamu ya nne mkoani Shinyanga mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani). (Picha na Suleiman Abeid)
Mtoto akipatiwa chanjo ya Polio (Picha kwa hisani ya Mtandao).