March 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chanjo ya polio kuwafikia watoto 146,960 Ilemela

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kufanya kampeni maalumu ya chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10,katika mikoa saba ikiwemo Mwanza,itakayofanyika kwa siku nne kuanzia Machi 24 hadi 27 mwaka huu.

Kupitia kampeni hiyo ambayo ni sehemu ya mpango wa kitaifa yenye lengo la kuimarisha kinga ya watoto dhidi ya ugonjwa huo hatari, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza inatarajia kuwafikia na kuwachanja chanjo ya polio watoto takribani 146,960 wenye umri chini ya miaka 10.

Hayo yamebainishwa Machi 17,2026 na Mratibu wa chanjo wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Shamte Almas,wakati akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uelewa wa pamoja wahudumu wa afya pamoja na wataalam mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya zoezi la utoaji chanjo hiyo.

Mafunzo hayo yametolewa kwa washiriki 663,wakiwemo watoa huduma, watakwimu na wahamasishaji (viongozi wa serikali za mitaa),kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya na mitaa yote 171.

Shamte amesema,wametoa mafunzo kwa wahamasihaji, watakwimu na watoa chanjo juu ya umuhimu wa chanjo ya polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10,ili kuwakinga na virusi hatari vya polio aina namba mbili ambavyo vimegundulika katika mkoa wa Mwanza.

“Chanjo hiyo itatolewa kwa watoto katika maeneo yote ya halmashauri ikiwemo nyumbani, shuleni na sokoni,ili kuhakikisha watoto wote wanaostahili kupata chanjo wanapatiwa,”amesema Shamte.

Muuguzi kutoka kituo cha Afya Buswelu pia ni mtoa chanjo,Doreen Mangia,amesema,kufuatia zoezi hilo watahakikisha kila anayestahili kupata chanjo ana patia huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kupata uelewa wa chanjo ya polio nOpV2 na umuhimu wake kwa watoto,katika kuwakinga na virusi hatari vienezavyo ugonjwa wa polio.

Kwa upande wake Mhamasishaji kutoka mtaa wa Kahama,Dorothy Ringo,amesema kupitia mafunzo hayo wamepata ulewa kuhusu madhara ya ugonjwa wa polio,hivyo atawaelimisha wananchi wa mtaani kwake umuhimu wa chanjo hiyo kwa watoto na kuhakikisha wote waliokusudiwa wanaipata.