Judith Ferdinand
Katika maeneo mengi ya masoko, stendi, na mikusanyiko mingine ya watu, kwa muda mrefu tumeshuhudia akinamama wengi wakiendelea na shughuli zao za biashara wakiwa na watoto wachanga.
Hali hii si tu kwamba inahatarisha usalama na makuzi bora ya watoto, bali pia inapunguza ufanisi wa kina mama katika kutekeleza majukumu yao ya kiuchumi.
Kauli hii inaungwa mkono na Glory John,mjasiriamali katika soko la Kiloleli, wilayani Ilemela mkoani Mwanza ambaye pia ni mama wa watoto wawili huku mmoja mwenye miaka mitatu na mwingine wa mwaka mmoja.

Akizungumza na Majira Glory,anasema kuwa ukosefu wa vituo vya malezi (day care) katika maeneo ya mikusanyiko ni changamoto kwa akina mama wanaojitafutia riziki.
Glory anasema,baadhi ya wajasiriamali wanawake hawana uwezo wa kifedha kuwalipia watoto wao huduma katika vituo vya malezi binafsi, wala kuwaajiri wasaidizi wa nyumbani (wadada wa kazi). Hali hii huwalazimu kuwapeleka watoto wao sokoni au maeneo ya kazi, jambo linalowaathiri moja kwa moja katika utendaji wao wa kazi.
“Unapokuwa sokoni, unaweza kuwa unamhudumia mteja, ghafla mtoto anaanza kulia au kutoroka,unalazimika kumuacha mteja au hata kufunga biashara kwa muda kumtafuta mtoto.Mfano mtoto wangu mkubwa alikuwa anatoroka mara kwa mara hivyo nalazimika kufunga biashara na kuanza kumtafuta .Wakati mwingine inabidi kuwalipa watu wanisaidie kumtafuta, hali inayochangia kupunguza kipato,” anasema Glory.
Anaeleza kuwa aliamua kumpeleka mtoto wake wa kwanza, mwenye umri wa miaka mitatu, katika kituo cha malezi binafsi ili kupunguza usumbufu aliokuwa akiupata sokoni. Hata hivyo, anasema uamuzi huo aliweza kuutekeleza kwa msaada wa mume wake.
Anaeleza kuwa kuna kina mama wengi ambao hawana msaada na wanategemewa pekee yao kuendesha maisha ya familia, jambo linalowaweka kwenye wakati mgumu zaidi.
“Mtoto mdogo naye si rahisi kuwa naye sokoni. Mara atake kubebwa, mara aanze kulia, na kama tunavyojua watoto wanahitaji muda wa kucheza, kupumzika kwenye mazingira tulivu,lakini haya yote hayapo katika mazingira ya masoko,” anasema Glory.
Kutokana na hali hiyo, Glory anatoa wito kwa Serikali na wadau wa maendeleo kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya malezi vya gharama nafuu katika maeneo ya mikusanyiko ya watu, hususani kwenye masoko na vituo vya biashara.
Anaamini kuwa uwepo wa vituo hivyo utasaidia kuhakikisha usalama na malezi bora kwa watoto, huku akinamama wakiweza kushiriki shughuli za kiuchumi kwa amani na ufanisi zaidi.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Pamela Kijazi,anasema kuwa changamoto ya kina mama wanaofanya biashara katika maeneo ya masoko, stendi na mikusanyiko mingine ya watu wakiwa na watoto wao imekuwa ni jambo linalohitaji suluhisho la muda mrefu na endelevu.
Kijazi anasema,kwa muda mrefu, akinamama wengi wamekuwa wakilazimika kuendelea na biashara huku wakiwa na watoto wachanga na wengine wenye umri chini ya miaka mitano,hali inayohatarisha usalama na makuzi bora ya mtoto, pamoja na kupunguza ufanisi wa mzazi katika shughuli za kiuchumi.
Nini suluhisho
Ujenzi wa vituo vya malezi katika masoko na maeneo ya mikusanyiko ndio suluhisho la watoto kupata malezi na wakina mama kupata fursa ya kufanya shughuli za kiuchumi kwa ufanisi.
Kijazi anasema,kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Ilemela imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba masoko yote mapya yanayojengwa yanakuwa na vituo maalum vya kulelea watoto mchana.
Anasema,vituo hivyo vitakuwa mahali salama ambapo watoto wataweza,kupata malezi bora kutoka kwa walezi waliobobea,kushiriki michezo,ujifunzaji pamoja na kupata lishe bora kwa afya na ukuaji wa mtoto.
“Kwa watoto wanaonyonya, kutakuwepo na maeneo maalum ya kunyonyeshea.Lengo ni kumuwezesha mzazi, hasa mama mfanyabiashara, kuendelea na shughuli zake huku mtoto akiwa salama na akipata huduma stahiki,”anasema Kijazi.
Mbali na mpango huo wa kujenga vituo vya malezi katika masoko mapya,pia Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na wadau ilianzisha vituo vya kulelea watoto katika jamii, ambavyo kwa sasa vipo takribani 17 kwenye mitaa mbalimbali ya manispaa hiyo.
Anasema,vituo hivyo vinapatikana hadi kwenye maeneo ya mialo, ambapo wazazi wengi hujihusisha na biashara ya mazao ya uvuvi.
Huku akisisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto wao katika vituo hivyo wanapokwenda kufanya shughuli zao za kiuchumi kwani mtoto anapokuwa kwenye kituo hicho atapata ulinzi,chakula chenye lishe bora pamoja na malezi kwa mujibu wa miongozo ya kitaalamu ya malezi na makuzi ya awali ya watoto.
“Mzazi anapomaliza shughuli zake za siku,atamchukua mtoto na kurejea naye nyumbani, kwa mujibu wa utaratibu wa kituo.Natoa wito kwa wazazi wote hasa kina mama wanaofanya shughuli za uchumi katika masoko, stendi, maeneo ya mialo na sehemu zingine zenye mikusanyiko ya watu, watumie huduma hizi zilizopo kwa ajili ya watoto wao,”amesema Kijazi na kuongeza:
“Kwa kufanya hivyo, mzazi atakuwa na uhakika wa usalama na ustawi wa mtoto wake, huku akiendelea kufanikisha malengo yake ya kiuchumi kwa ufanisi zaidi,”.

Jitihada za TAHEA katika malezi ya watoto
Mratibu wa Miradi ya Malezi ya Watoto wa shirika la Uchumi wa Nyumbani (Tanzania Home Economics Organization-TAHEA) Mwanza,Damas Joachim,anasema katika kuhakikisha watoto hususani waliochini ya umri wa miaka 8, wanapata malezi bora walianzisha vituo vya kijamii vya malezi 12 wilayani Ilemela na sasa wameanza ujenzi wa kituo cha malezi wilayani Misungwi.
Damas anasema,vituo hivyo 12 kwa Wilaya ya Ilemela wamejenga katika mitaa iliopoa katika Kata za Kayenze,Sangabuye,Bugogwa na Shibula kunakofanyika shughuli za uvuvi.
Sababu za TAHEA kuanzisha vituo katika maeneo hayo
Damas anasema,sababu walibaini maeneo hayo hayana mfumo mzuri wa maadili na malezi ya watoto kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kutojipanga kuanzisha familia au makazi ya kudumu.
“Mtu anaenda kwa lengo za shughuli za uvuvi na kuanzisha makazi ya muda mfupi lakini akifika kule anapata mwanamke wanaanzisha familia kwa kuzaa watoto kitendo ambacho wanakuwa hawajakipanga,hivyo mtu akiona familia imeanza kuwa kubwa anaona bora ajenge na kukaa hapo,katika mazingira ya namna hiyo malezi yanaathirika zaidi,”anasema Damas na kuongeza:
“Pia maeneo ya ziwani mfumo wa maisha hautoi nafasi ya malezi bora kwa watoto kwani muda mwingi wanatumia katika mabanda ya “video”,ata kwenye mwambao wa ziwa unakuta watoto wadogo wenye umri wa miaka miwili mpaka miwili na nusu,wamezagaa katika maeneo hayo na hawana uangalizi mzuri na kule unakuta watu wazima wengine wanaoga hadharani huku watoto hao wakiwashuhudia,”.
Damas anasema,lengo la kuanzisha vituo hivyo vya Jamii vya malezi ya watoto wadogo mchana ni kuwapatia watoto wadogo fursa ya kujifunza kwa njia ya michezo (play based learning) ili waweze kupata ukuaji sahihi na kufikia utimilifu wao.
Pia kuwapa wazazi na walezi muda wa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zao za uzalishaji mali pasipo wasiwasi wakati watoto wao wakipata malezi mbadala kwenye mazingira salama.
Hata hivyo msingi wa taifa bora ni lenye watoto ambao wanapata huduma ya malezi bora kwa usawa bila kujali hali zao na za wazazi wao.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria