Na Fresha Kinasa, TimesMajira Online,Musoma.
Kitogoji cha Busumi, Jimbo la Musoma Vijijini,mkoani Mara,wavuvi 20,wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi(Busumi Fishing Cooperative Society),wamepata mkopo wa milioni 117,usio na riba kutoka kwa serikali,kwa ajili ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.
Awali wavuvi hao kutokana na kufanya shughuli za kuhama hama,walikuwa hawakopesheki na taasisi za kifedha,hivyo kushindwa kufanya shughuli ya uvuvi kwa ufanisi na tija.Hali iliyochangia kufanya uvuvi wa mazoea ambao uliwapatia kipato ambacho wakati mwingine akikukidhi mahitaji ya familia zao.
Juma Bwire ni Mkazi wa Kitongoji cha Busumi, akizungumza Agosti,20,2024 , na TimesMajira online, ameeleza kuwa,kabla ya kupata mkopo huo wa serikali,walikuwa hawakopesheki.Ikitokea mvuvi kapata mkopo, basi alikopa mwenyewe katika taasisi ya fedha anayoijua na kurejesha kwa utaratibu wake binafsi.
Lakini hatua hiyo ya kupata mkopo wa serikali kwa ajili ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ,utawafanya wavuvi wafanye shughuli za uvuvi wa kisasa ambao utawapa faida kiuchumi na kuondokana na uvuvi usio na tija.
“Utakuwa mchango katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu. Serikali iendelee kutoa mikopo hii nafuu, ambayo itakuwa chachu ya kuleta mafanikio katika kuongeza mapato na kubadili hali ya uchumi kwa wavuvi wengi,”amesema Jesca Nyasatu Mwananchi anayeishi katika Kitongoji cha Busumi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Agosti 20, 2024,imeeleza kuwa kiasi hicho cha fedha cha milioni 117, kilichotolewa kwa Chama Cha Ushirika wa Wavuvi Busumi, ni kwa ajili ya kupata vizimba vinne (4), vifaranga vya samaki, chakula cha samaki na bima ya ufugaji wao wa samaki.
Sehemu ya taarifa hiyo , imeeleza kuwa wataalamu wa usukaji wa vizimba walikamilisha kazi zao, na juzi(Agosti 18,2024),vizimba hivyo vilipelekwa ndani ya Ziwa Victoria ,eneo la kijiji cha Suguti Jimboni humo.
“Uvuvi wa vizimba upande wa Jimbo la Musoma Vijijini, umeanza kwa mafanikio,kwa maeneo ya Vijiji vya Kigera (Etuma), Bwai Kwitururu na Suguti.Wavuvi wa maeneo mengine wamehamasika, hivyo wanajitayarisha kutuma maombi serikalini ya mikopo ya ufugaji kwa njia ya vizimba,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto