December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chama cha ushirika SONAMCU kinavyowatajirisha wakulima Ruvuma

Na Stephano Mango,TimesMajira Online,Songea

CHAMA cha Ushirika ni “Muungano wa watu waliojiunga pamoja, kwa hiari, kwa madhumuni ya kufanikisha mahitaji yao kwa kuanzisha na kumiliki chombo chao kidemokrasia na kuchangia mtaji unaohitajika kwa usawa na kukubali kuyakabili matatizo na kupata manufaa kutokana na shughuli zake ambazo wao hushiriki kikamilifu.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkongogulioni Wilaya ya Namtumbo kuhusu umuhimu wa kuuza mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani

Katika vyama vya ushirika wanachama wanakuwa na uwezo mkubwa wa kutatua matatizo yao ya kiuchumi na kijamii kwa kutumia juhudi zao za pamoja katika kufikia malengo ambayo yasingefikiwa kwa juhudi za mtu mmoja mmoja.

Jukumu kuu la ushirika katika mazingira ya uchumi wa soko huru, Vyama vya ushirika ni miongoni mwa watekelezaji wengi wa shughuli za biashara kwenye soko.

Wanaushirika wanahitaji vyama vilivyoundwa katika umoja wa vikundi mbalimbali vya wazalishaji wadogo kwa lengo la kuunganisha nguvu za rasilimali zao katika kuendesha shughuli zao za biashara kwa ufanisi ili waweze kuhimili ushindani wa wafanyabiashara wengine katika soko

Kwa muktadha huo chama kikuu cha Ushirika SONAMCU LTD ambacho kiliandikishwa tarehe 30.01.2003 na kusajiliwa kwenye daftari la Serikali kwa kupewa namba ya Usajili 5491.

Chama hiki kinatokana na vyama vikuu vya ushirika tangulizi vitatu (3) ambavyo vilikuwa vinajulikana kama Songea Agricultural Cooperative Union (SAMCU) kilianzishwa mwaka 1994,

Wakwanza kulia ni Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akimueleza jambo Meneja wa SONAMCU Juma Mwanga alipotembelea kiwanda cha vifungashio kilichopo Namtumbo hivi karibuni.

Ruvuma Cooperative Union (RCU) kilianzishwa mwaka 1989 pamoja na Ngoni matengo Tabacco Growers Cooperative Union (NGOMAT) kilichoanzishwa mwaka 1936.

Chama kikuu kina wanachama 46 wa vyama vya msingi kati ya hivyo 35 vipo wilaya ya namtumbo, vyama 5 vipo, Songea vijijini, vyama 2 Songea Manispaa, vyama 3 mbinga vijijini na chama 1 madaba.

Meneja wa SONAMCU Juma Mwanga akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake hivi karibuni anasema kuwa chama kilianzishwa kwa madhumuni ya kusimamia na kuratibu masoko ya mazao ya Tumbaku na mazao mchanganyiko katika maeneo ya wilaya ya Namtumbo na Songea.

Mwanga anasema kuwa Chama kikuu cha ushirika SONAMCU LTD kilianzishwa kwa madhumuni ya kuratibu na kusimamia shughuli kama vile

Kusimamia na kuratibu uendeshaji wa shughuli za kila siku za vyama vya msingi (amcos) ,Kutoa elimu ya ushirika na ujasilia mali kwa vyama vya msingi wanachama.

Meneja wa SONAMCU Juma Mwanga akielezea mafanikio ya chama hicho.

Kutafuta masoko ya nje ya nchi ya mazao ya wakulima wanachama, Kuhamasisha wakulima kukusanya na kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na Kutoa mikopo midogo kwa wanachama kwa ajili ya kuendesha shughuli za AMC

Chama kikuu cha ushirika SONAMCU LTD kimeundwa na mkutano mkuu kama chombo kikuu cha kutoa maamuzi ya chama ikifuatiwa na Bodi ambayo inasimamia shughuli za kila siku za kitendaji kwa niaba ya wanachama, pia wanafuata watendaji wakiongozwa na meneja mkuu ambayo wanatekeleza majukumu ya kila siku kwa niaba ya Bodi.

Chama kikuu cha ushirika SONAMCU LTD kinamiliki mali zifuatazo ambazo zinamilikiwa na wanachama kwa asilimia 100. Kiwanda cha Tumbaku cha SONTOP. Hotel ya Angon Arms. Maghala.Chuo cha ushirika na Majengo mbalimbali

Mwanga anaeleza zaidi kuwa katika kuhakikisha chama kinajiendesha chenyewe pasipo kutegemea ushuru utokanao na mauzo ya mazao ya wakulima chama kina mipango mbalimbali

Zao la ufuta ambao ni miongoni mwa mazi yanayouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani mkoani Ruvuma, mazao mengi ni mbaazi na ufuta.

Ikiwemo kuanzisha kiwanda cha vifungashio kinachojengwa katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ambacho kitaajili watu 500. Kiwanda hiki kinatarajiwa kuanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwaka 2022

“Katika mwaka wa fedha 2022/2023 chama kinampango wa kununua na kuanzisha mashamba yenye ukubwa wa ekari 3000 mashamba ambayo yatatumika kwa shughuli za kilimo hasa yale yanayouzwa kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghalani yaani Ufuta, Soya na mbaazi”anasema Mwanga

Chama kina mpango wa kutafuta masoko ya zao la Tumbaku ambapo kwa hali ya sasa uzalishaji wa Tumbaku ni tani 500 tu ambapo wakulima wanauwezo wa kulima zaidi ya tani 10,000.

Kwa kushirikiana na Ofisi ya Bodi ya Tumbaku Tanzania chama kipo katika mazungumzo ya kutafuta wanunuzi wengine wa Tumbaku badala ya kutegemea mnunuzi mmoja ambaye ni kampuni ya PREMIUM ACTIVE TANZANIA LTD.

Katika mwaka wa fedha 2022/2023 cha kina mpango kukodisha au kutafuta mbia wa kuendesha miradi iliyosimama kama vile hotel ya Angon Arms pamoja na chuo cha ushirika kilichopo wilaya ya Namtumbo.

Akielezea kuhusu mpango wa Stakabadhi ghalani alisema kuwa mkoa wetu wa Ruvuma uliingia katika mfumo wa Stakabadhi ghalani mnamo mwaka 2019.

Baada ya kupokea waraka wa mrajis wa vyama vya ushirika Tanzania mnamo mwaka 2019. Hivyo chama kilipokea mwongozo kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa juu ya usimamizi na uratibu wa masoko ya mazao ya Ufuta,Soya na mbaazi.

Anasema kuwa mafanikio waliyoyapata kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wakulima wanakutanishwa na wanunuzi hivyo kuwafanya wawe na maamuzi juu ya kuuza mazao yao kwa umoja wao.

Mfumo wa stakabadhi ghalani umepelekea kuwepo kwa matumizi ya vipimo halali vya wakulima kwani wanunuzi hutumia mizani iliyohakikiwa na wakala wa vipimo badala ya majagi yaliyokuwa yanatumika kabla ya mfumo.

Pia mfumo umepelekea upatikanaji wa Tozo za serikali (Ushuru) kwa njia rahisi ukilinganisha kabla ya mfumo hii imepelekea kuongeza kwa mapato ya Halmashauri.

Kuongezeka kwa bei ya mazao ya Ufuta, Soya na mbaazi hii imetokea na kuongezeka kwa wanunuzi ambao wanashiondanishwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kutoa bei kubwa kwa wakulima.

Kufufuka kwa vyama vya ushirika toka vyama 24 vilivyokuwa vinauza tumbaku tu hadi vyama 63 ambavyo viliuza mazao ya Ufuta, Soya na Mbaazi ambayo yanauza kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Kuongezeka kwa uzalishaji mazao ya Ufuta, Soya na Mbaazi hii imetokana na wakulima kuwa na uhakika wa masoko ya mazao hayo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Moja ya minada ya zao la soya kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani uliofanyika eneo la Lilambo wilayani Songea

Anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021,kupitia zao la ufuta,wakulima waliuza kilo 19,163,454 na kufanikiwa kupata zaidi ya shilingi bilioni 45,huku Halmashauri zikipata mapato ya zaidi ya bilioni 1.9,SONAMCU ilipata zaidi ya milioni 574 na vyama vya msingi zaidi ya shilingi bilioni1.341.

Katika kipindi hicho cha miaka mitatu katika zao la soya ziliuzwa jumla ya kilo 5,550,290 na wakulima kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 4.925,mapato ya Halmashauri zaidi ya shilingi milioni 156,SONAMCU zaidi ya milioni 84 na mapato ya vyama vya msingi ni zaidi ya milioni 194.

Anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021 katika zao la mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ziliuzwa kilo 4,920,996 ambazo ziliwaingizia wakulima zaidi ya shilingi bilioni nne,Halmashauri ilipata zaidi ya shilingi milioni 143,SONAMCU ilipata zaidi ya milioni 59 na vyama vya msingi vilipata zaidi ya shilingi milioni 129.

Anasema kuwa zipo changamoto ambazo zinawakabili ikiwemo kukosekana kwa elimu ya Stakabadhi ghalani kwa wakulima hasa katika maeneo ya wilaya ya Nyasa, Mbinga na Madaba.

Kuongezeka kwa mgogoro wa kimaslahi kwa wafanyabiashara wanaopinga mfumo kutumia wanasiasa ili kuzuia mfumo usifanye kazi hii inapelekea kuwepo na utoroshwaji mkubwa wa mazao hasa zao la Soya kuuzwa nje ya mfuko wa stakabadhi ghalani na kupelekea vyama na Halmashauri kukosa mapato.

Kuwepo kwa miundombinu isiyo rafiki hasa barabara katika baadhi ya maeneo hii imesababisha wakulima kushindwa kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi.

Mabadiliko ya matamko ya viongozi juu ya mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa ni ya ghafla hii inapelekea vyama kutokuwa na uhakika wa maandalizi ya masoko kwa msimu unaofuata.

Kupunguza kwa uzalishaji wa Tumbaku toka 9000 kwa mwaka 2020 hadi tani 500 kwa mwaka 2021, hii imetokana na Tanzania kujitoa kwa uanachama wa COMESA ambayo nchi ya Misri ndiyo mnunuzi mkubwa wa Tumbaku ya Moshi ambayo inazalishwa katika mkoa wa Ruvuma.

Meneja huyo anasema kuwa ili waweze kufanikiwa zaidi wanaiomba serikali ya mkoa ikishirikiana na Ofisi ya Bodi ya TumbakuTanzania (TTB) kusaidia upatikanaji wa wanunuzi wa Tumbaku ili kuongeza uzalishaji wa zao la Tumbaku.

Pia tunaomba Serikali kupitia Ofisi ya mkuu wa Mkoa kuongezea msisitizo juu ya uimarishaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwani umeleta tija kwa wakulima wa mkoa wa Ruvuma.

Tunaiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo kuingia mkataba wa muda mrefu nan chi ya India (Biliteral Trade) juu ya uuzaji wa zao la Mbaazi ili kuwafanya wakulima a Mbaazi wawe na uhakika wa soko.