Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online TV, Dae es Salaam.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wafanyabiashara kuheshimu sheria za ulipaji kodi kwa kutoa risiti na kulipa kodi pindi wanapouza bidhaa zao kwa kutumia mashine za kieletroniki (EFD).
Pia amewaonya wafanyabiashara kuepuka migomo wayofanywa pindi kunapofanyika mabadiliko ya makadilio ambayo hawaridhishwi nayo na kudai kuwa ni vyema wakafika kwenye mamlaka husika ili kutatua changamoto zao.
Chalamila, ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua wiki ya mbio za mashine za kielektroniki (EFD), ambazo zimeanza rasmi Septemba 23 hadi 30 mwaka huu uwanja vya Jakaya Kikwete jijini humo.
“Najua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), haiwezi kupendwa..hivyo msipoteze muda kwenye kupendwa kwa sababu taifa linahitaji kodi na ndio mfumo wa taifa letu kwenda mbele, achaneni na migomo ambayo si afya ni vizuri mkalilia mabadiliko ya sheria na mifumo ya kodi iboreshwe kuliko kuandamana,” amesema Chalamila.
Pia ameitaka TRA, kuendelea kutoa elimu kwa walipa kodi, ili kuepusha migomo isiyokuwa ya lazima.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha kutoka TRA, Dinah Edward, akimwakilisha Kamishina Mkuu, Alphayo Kidata, amesema Mkoa wa kikodi wa Ilala ndio unaongoza kwa ukusanyaji wa mapato nchini.
“Mkoa wa kikodi wa Ilala ni mkubwa na unaongoza kwa makusanyo ya mapato kwa Mkoa wa Dar es Salaam salaam vilelevile kwa nchi nzima kwa ujumla,tunaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya ulipaji kodi katika maeneo yenye wafanyabiashara,” amesema Dinah.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiasha wa Kariakoo, Martin Mbwana aliwaahidi viongozi wa Mkoa wa Dar es Salam kuwa, wataenda kushirikiana na TRA katika kuhakikisha wanatoa na kudai risiti wakati wakiuza na kununua bidhaa ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Hata hivyo mwakilishi wa kampuni ya uuzaji wa mashine za EFD na mashine za risiti za vituo vya uuzaji wa mafuta nchini Radix , Dora Lusingu amesema katika kutambua umuhimu wa ulipaji kodi wataendelea kuwahimiza wafanyabiashara kutumia mashine hizo.
“Wafanyabiashara msiogope kutumia mashine za EFD kwasababu zinasaidia ulinzi wa biashara yako pia kujua mapato yako unayoyaingiza mwisho wa mwezi na wa mwaka,zinasaidia kutunza kumbukumbu za biashara yako, kujua biashara yako inaendaje pamoja na kujenga uchumi wa taifa letu,” amesema Dora.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ambaye ndiye alitoa tuzo kwa washindi watano wa mwanzo wa mbio hizo, katika makundi manne, alivishukuru vyombo mbambali vya habari kwa kuendelea kutoa taarifa za uhamasishaji wa wiki ya EFD pamoja na kuwashukuru wananchi waliojitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio za EFD Marathon, zilizoandaliwa kwa lengo la kutoa elimu.
Wiki ya mashine za risiti za kielektroniki (EFD), imeanzishwa na TRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, kwa ajili ya kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za kutoa risiti, kujenga uhusiano kati ya TRA na wafanyabiashara sambamba na utoaji wa elimu ya kodi kwa wananchi na wafanyabiashara katika mikoa ya kikodi ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili