Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewatoa hofu madereva wa vyombo vya moto vya magurudumu mawili pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’na wamachinga wa Mkoa wa Dar es Salaam, katika Wilaya ya Ilala, kuwa Serikali ipo pamoja nao na itaendelea kuwawekea mazingira rafiki ya kufanyia shughuli zao.
Akizungumza mjini Dar es Salaam , katika mkutano wa machinga na ‘Bodaboda’ uliofanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja, ulikuwa na lengo la kusikiliza kero zao na kufanyiwa utatuzi, Chalamila amesema wamachinga na madereva wa bodaboda ni watu muhimu katika nchi hii.
Chalamila amesema, kati ya mambo ambayo Serikali itaangalia katika kuhakikisha inawawekea mazingira rafiki madereva bodaboda ni pamoja na kupatiwa bima itakayo warahisishia hata pale wanapopata majanga ya ajali au kuibiwa pikipiki pamoja na bima ya matibabu ili familia zao zisipate shida.
“Baada ya kuingia Dar nimegundua wamachinga na bodaboda wana mateso sana,hawa madereva bodaboda wanaonekana wamekabidhiwa hizo bodaboda lakini jioni wana marejesho, sasa tusiwaumize bila msingi, kwani pia wanaonekana hata bima hawana hivyo kama Serikali inabidi tuliangalie hili ili inapotokea wamepata ajali au kuibiwa pikipiki zao basi familia zao zisiangaike,” amesema Chalamila.
Aidha, Chalamila alikemea vitendo vya baadhi ya kampuni kubugudhi madereva bodaboda pindi wawapo barabarani na kuwanyang’anya kwa madai kuwa wamepaki vibaya na kuwatoza kiasi kikubwa cha fedha.
“Lakini jambo lingine ni hawa bodaboda wakipaki pikipiki zao tu barabarani yanakuja makampuni na kuwanyang’anya kuwa wamepaki vibaya na kuwatoza kiasi kikubwa cha fedha..hii siyo sahihi na jambo hili tunalifanyia kazi, kwa sababu pia Kuna kijana mmoja alikuwa anadaiwa milioni 1.2 sasa kwa kuangalia hapo kwenye pikipiki atapata nini?,”amesema Chalamila.
Hata hivyo kwa upande wa wamachinga, Chalamila amesema, wao kilio chao kikubwa ni sehemu yenye mazingira rafiki ya kufanyia biashara zao na kupata wateja, ambapo alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo kuangalia namna ya kuandaa utaratibu wa kuwepo kwa minada angalau mara 3 kwa wiki katika maeneo ya wazi.
Pia aliwataka wamachinga na madereva bodaboda kutosikiliza upotoshwaji juu ya masuala ya bandari na kusema kuwa, kuna watu wapo kwa ajili ya kuharibu na wao kama Serikali hawapo tayari, kwani suala ya uwekezaji katika bandari ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi na si vinginevyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kwazi nzuri ambayo ameendelea kufanya ya kuhakikisha anatekeleza yale yote aliyoahidi katika Wilaya hiyo.
Mpogolo amesema, hadi sasa Wilaya ya Ilala imenufaika katika katika maeneo mengi ikiwa pamoja na upande wa elimu, afya na biashara.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Zungu amesema, bodaboda na wamachinga ni watu muhimu na wanaopaswa kusikilizwa na kuwekewa mazingira salama kwa ajili ya kufanyia shughuli zao.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato