December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila jana katika Kijiji cha Hatwelo, Kata ya Ijombe mkoani humo katika tamasha la sita la Jinsia ngazi ya Wilaya lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)

Chalamila awaonya wanaume wanaowanyanyasa wajane

Na Esther Macha,Timesmajira, Online,Mbeya.

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewaonya wanaume wanaonyanyasa wajane na Watoto katika masuala ya mirathi pindi wanapoondokewa na wapendwa wao kuwa tabia hiyo haitavumilika kwa atakaowabainika.

Chalamila ametoa rai hiyo jana katika Kijiji cha Hatwelo, Kata ya Ijombe mkoani humo katika tamasha la sita la Jinsia ngazi ya Wilaya lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) .

Amesema hivi sasa Mkoa wa Mbeya umejipanga kukabiliana na wanaume wanaowanyanyasa wajane na watoto kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria .

Chalamila amesema katika kukabiliana na hilo Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria wanawake wamefungua ofisi zao jijini Mbeya ili kuweza kuwasaidia wajane hao katika masuala ya kisheria.

“Mwanaume atakayebainika au kuthubutu kumnyanyasa mjane na watoto wa marehemu kwenye mirathi ajiandae kurithiwa yeye  kwanza kabla ya kuwasumbua wasiohusika ,tayari kama Mkoa tumeshaongea na wanasheria wanawake ambao wamekubali kuja Mbeya na tayari wameshafungua ofisi hapa,”amesema  Chalamila

Amesema  ili kuendelea kupunguza manyanyaso ya kijinsia kwenye jamii ni lazima elimu iendelee kutolewa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maazimio ya Beijing yanashushwa hadi ngazi ya chini jambo litakalochangia  kuikwamua jamii kiuchumi.

Amesema elimu juu ya mitazamo hasi kuhusu wanawake iendelee kutolewa kwani baadhi ya jamii bado zinaamini kuwa mwanamke hastahili kumiliki ardhi, kupata mirathi, kukopa benki na kupata nafasi ya uongozi.

Aidha ametoa wito kwa wanawake kuacha kuvumilia manyanyaso kutoka kwa wanaume bali wapaze sauti kwa kuwafikisha katika vyombo vya dola ili sheria iwachukulie hatua stahiki na kukomesha kabisa tabia hiyo.

Aidha amewataka Wanawake kuacha kujirahisisha pindi wanapotaka nafasi za uongozi kwa kukubali kutoa rushwa ya ngono ili waweze kupatiwa nafasi wanayoitaka.

Mjumbe wa Bodi ya TGNP, Jovitha Mlay amesema katika tamasha hilo washiriki zaidi ya 300 walijitokeza wakiwemo kutoka mikoa tisa na halmashauri 12 nchi nzima ambao wanafanya kazi na mtandao huo.

Amesema jambo kubwa lililojadiliwa ni kuielimisha jamii kuhusu vipaumbele vilivyopo kwanye mazingira yanayowazunguka wanawake yanayoweza kuingizwa kwenye bajeti yenye mlengo wa kijinsia kupitia mikutano ya vitongoji, vijiji, kata na halmashauri.