January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chalamila ataja mambo yanayothibitisha uzalendo na uchapakazi wa Rais

Na Ashura Jumapili,TimesMajira Online,Bukoba

Mkuu wa Mkoa wa Kagera ,Albert Chalamila,ametaja mambo mbalimbali yanayothibitisha uhodari,uzalendo na uchapakazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasaan ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Chalamila,ameyataja mambo hayo katika hafla ya kumpongeza Rais Samia kwa kazi ambazo amezifanya kwa kipindi cha miaka miwili tangu alipoingia madarakani kwa kuapishwa Machi 19,2021.

Ameeleza kuwa wakati Rais anaingia madarakani alisikia kilio cha wazazi waliokuwa wakilia wakati wa kuchangia michango kwaajili ya kujenga vyumba vya madarasa kila mwaka.

Ambapo kwa awamu ya kwanza alitoa kiasi cha zaidi ya bilioni 17 kwa ajili ya kujenga madarasa 881 na awamu ya pili kiasi cha bilioni 10.2 kwa ajili ya vyumba 514.Chalamila ameeleza kuwa pia alitoa onyo kwa viongozi wa chini kutowachangisha wazazi michango inayohusu ujenzi wa miundombinu ya shule.

Pia ameeleza.kuwa katika sekta hiyo ya elimu Rais amefuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili watoto wote waweze kupata elimu ya sekondari hasa ya juu ili wajiunge na elimu ya vyuo vikuu na kuweza kuwa mahiri kwa kutimiza ndoto zao.

Pamoja na hayo Chalamila ameeleza kuwa Mkoa huo unapokea kiasi cha bilioni 1.6 kila mwenzi kutoka serikalini kwaajili ya kulipia ada na posho za watumishi wa sekta ya elimu.”Rais amejenga shule 12 zenye hadhi katika Mkoa wa Kagera zenye thamani ya bilioni 8 na wanufaika wakuu ni wazazi ambao watoto wao wanasoma katika shule hizo,”ameeleza Chalamila.

Vilevile ameeleza kuwa Rais ameamua kujenga tawi la cyhuo Kikuu cha Dar-es-Salaam katika eneo la Kangabusharo na Itahwa lenye ukubwa wa hekali 314 na awamu ya kwanza ametoa kiasi cha bilioni 17.5 ili ujenzi uanze na kuleta chachu ya uchumi katika mkoa.

“Juni Mosi mwaka huu ujenzi wa chuo hicho utaanza rasmi na fursa za uchumi zitafunguka kwa wakazi wa Kagera,naomba kufunguliwa kwa baadhi ya vyuo zilivyofungwa katika Mkoa wa Kagera ili kuweza kuufanya mkoa huu kuendelea kung’ara katika sekta ya elimu,”ameeleza Chalamila.

Katika sekta ya afya ameeleza kuwa Rais Samia ,ameweka historia katika Mkoa huo kwani tangu uhuru hapakuwa na hospitali za Wilaya zilizokuwepo zilikuwa za taasisi za kidini kwa kutoa zaidi ya bilioni 40 ambazo zimegawanyika katika sekta ya afya kwa kujenga zahanati,vituo vya afya na hospitali za wilaya.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa pia ameleta mashine katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo CT-SCAN yenye thamani ya bilioni 1.8 na kuwaondolewa wananchi adha ya kwenda Bugando mkoani mwanza kwa kipimo hicho.

Katibu Tawala Mkoa wa Kagera (RAS ),Toba Nguvila,ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita inasimamia utekelezaji wa ilani ya mwisho katika utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025 ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa malengo ya Chama Cha Mapinduzi(CCM),katika kustawisha maisha ya watanzania na kutokomeza umasikini.

Nguvila, ameeleza kuwa serikali chini ya usimamizi wa Rais Samia, imeweza kutekeleza vyema ilani ya CCM ya mwaka 2020 kwa kutekeleza maeneo sita ya vipaumbele kama ifuatavyo kulinda na kuimarisha misingi ya utu,usawa haki na uongozi bora ili kudumisha amani umoja na mshikamano wa taifa.

Ameeleza kuwa pia kukuza uchumi wa kisasa fungamanishi jumuishi na shindani iliyojengwa katika misingi ya viwanda,huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.

Pia ameleta mageuzi ya kilimo ,mifugo na katika sekta uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.

Pamoja na kuimarisha upatikanaji bora wa huduma za afya,elimu, maji,umeme na makazi vijijini na mijini, kuchochea matumizi ya utafiti wa sayansi na teknolojiana, ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi.

Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera,Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ,Karim Amri ,amewataka viongozi wa serikali ngazi zote kutatua kero za wananchi na wasiwe miungu watu wasiopokea simu wala kutatua kero za wananchi.

Amri, ameeleza kuwa wakifanya hivyo wataweza kushinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao kwa kuwahudumia wananchi, ipasavyo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila, akizungumza katika hafla ya kumpongeza Rais Samia kwa kazi ambazo amezifanya kwa kipindi cha miaka miwili tangu alipoingia madarakani kwa kuapishwa Machi 19,2021.
Katibu tawala mkoa wa Kagera Toba Nguvila,akizungumza katika hafla ya kumpongeza Rais Samia kwa kazi ambazo amezifanya kwa kipindi cha miaka miwili tangu alipoingia madarakani kwa kuapishwa Machi 19,2021.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Karim Amri,akizungumza katika hafla ya kumpongeza Rais Samia kwa kazi ambazo amezifanya kwa kipindi cha miaka miwili tangu alipoingia madarakani kwa kuapishwa Machi 19,2021.
Viongozi wa dini waliohudhuria katika hafla ya kumpongeza Rais Samia kwa kazi ambazo amezifanya kwa kipindi cha miaka miwili tangu alipoingia madarakani kwa kuapishwa Machi 19,2021.