December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika

CHADEMA yafukuza wabunge wanne

Watuhumiwa kuvunja Katiba, kujeli na kupuuza maazimio ya Chama,
Spika akataa, ataka waendelee kuchapa kazi, mvutano washika kasi

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewafuta uanachama wa chama hicho wabunge wake wanne hivyo kuwafanya wakose sifa za kuendelea kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uamuzi huo umetangazwa jana na jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, wakati akitangaza maazimio yaliyofikiwa na Kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika mwishoni mwa wiki.

Mnyika amewataja wabunge ambao Kamati Kuu imeazimia kuwafuta uanachama kuwa ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Mbunge wa Moshi Vijiji, Anthony Komu, Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare na David Silinde.

Mnyika amesema katika azimo la kwanza la kikao hicho cha Kamati Kuu linawahusu Komu na Selasini. Amesema pamoja na wanasiasa hao kujipotezea sifa ya uanachama wao wenyewe, lakini wameendelea kutoa kauli za kejeli, kashfa na kupuuza maazimio ya chama.

“Na kwa sababu hiyo chama kimeamua kuwafukuza uanachama wa chama na Kamati Kuu ya Chama imeelekeza Katibu Mkuu wa Chama (Mnyika) kumuandikia Spika wa Bunge juu ya uamuzi huo,” amesema Mnyika na kuongeza;

“Tumesema pamoja na kwamba wamepoteza sifa ya uanachama kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ya Chama, sifa ya mwanachama wa CHADEMA kwa mujibu wa kifungu cha 5.1:5  mwanachama wa CHADEMA ni lazima awe anakubaliana na itikadi na falsafa ya Chama.”

Mnyika amesema Mheshimiwa Komu na Selasini wameshajitokeza kwenye vyombo mbalimbali vya habari na wakatangaza bayana kwamba hawakubaliani na itikadi na falsafa ya CHADEMA, bali  wanakubaliana na ya vyama vingine.

Amesema baada ya hapo wanasiasa hao wameendelea kufanya matukio mengine na kutoa lugha ya kejeli na kashfa na mambo mengine kwa viongozi wa chama.

Kutokana na hali hiyo, Mnyika alisema Kamati Kuu imefikia uamuzi wa kuwafuta uanachama.

Mnyika ametaja azimio la pili ambalo Kamati Kuu imelipitia ni kuhusu kuwavua uanachama, Silinde na Lwakatare,akisema sio tu wamekiuka maagizo ya chama, bali pia wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya habari na njia nyingine za mawasiliano kutoa maneno ya kashfa kejeli dhidi ya maazimio ya chama na viongozi.

Amesema kwa kuzingatia mambo hayo Kamati Kuu ya Chama imefikia uamuzi wa kuwafuta uanachama, kwani mbali na kukiukwa maagizo ya chama wameendelea kujitokeza kwenye vyombo vya habari na kutoa maneno ya kashfa kwa chama na viongozi wake kinyume cha taratibu za chama.

Jambo la tatu ambalo Kamati Kuu ilijadili kwa mujibu wa Mnyika ni kuhusu mjumbe wa Kamati Kuu, Mariam Msabaha, ambaye naye anadaiwa kushiriki kukiuka maagizo na makubaliano ya chama.

Mnyika amesema kwa kuwa mwanasiasa huyo ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, alitakiwa awe mstari wa mbele kuonesha mfano, lakini ameshindwa kufanya hivyo.

“Kwa hiyo Kamati Kuu imepitisha azimio la kumvua nyadhifa zake zote za uongozi alizonazo ndani ya chama na kubaki na nafasi aliyonayo ya Ubunge na atatakiwa kujieleza kwa Chama ni kwa nini asichukuliwe hatua zaidi kwa ajili ya ukaidi huo ambao ameuonesha kwa chama,” amesema Mnyika.

Wakati huo huo, Mnyika amejibu kauli iliyotolewa na Spika wa Bunge Job Ndugai, kuhusiana kuchukua posho kiasi cha sh.milioni 110 bila kuhudhuria vikao vya Bunge ambapo alifananisha kitendo hicho kuwa ni wizi sawa na wizi mwingine.

Akijibu kauli hiyo ya Spika Ndugai, Mnyika amesema madai haya ya Spika wa Bunge hayana ukweli.

“Kuhusu madai yaliyotolewa na Spika kwamba wabunge wa CHADEMA waliopewa posho za kujikimu kwamba ni wezi, madai haya ya Spika wa Bunge ni uongo, Chama kimetoa rai kwa wabunge kutokutelekeza yale ambayo Spika ameyasema, wabunge wa CHADEMA sio wezi,” Mnyika, Katibu Mkuu CHADEMA

Spka ndugai ameendelea kusisitiza wabunge wa CHADEMA kurudi bungeni haraka iwezekanavyo na fedha za posho walizolipwa akisisitiza kwamba fedha hizo hazitakatwa popote, isipokuwa wanatakiwa kuzirejesha ndipo wataelewana.

Spika awagomea CHADEMA

Katika hatua nyingine Spika wa Bunge, Ndugai amepinga uamuzi wa CHADEMA wa kuwafukuza uanachama wabunge wake wanne na amewataka kuendelea kuchapa kazi kama kawaida, huku akihoji mtu mmoja (Freeman Mbowe) anawezaje kufukuaza wabunge wote hao.

Spika wa Bunge, Job Ndugai,

Spika Ndugai amesema anachukua chama kama chake ikiwa ni pamoja na kuwatishia abunge. “Msiogope aliyewaapisha ni Bunge, huyo anayewafukuza ni nani? Mchape kazi zenu zenu kwani huyo aliyewafukuza anajua Novemba hatarudi Bungeni ndiyo maana anawatishia tishia, anafikiria anachokiamua ni sahihi,” amesema Spika Ndugai.

Amewataka wabunge hao kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge kama kwa kawaida na kumshauri msajili wa vyama vya siasa kuangalia vyama hivyo.

Kuhusu wabunge ambao wamekuwa wakiwasema wabunge waliofariki hivi karibuni kwamba walikufa kwa Corona, Spika Ndugai aliwataka waache hiyo tabia ili familia zao zitulie maana zipo kwenye majonzi, masikitiko.

Amesema ni jambo la kushangaza badala ya kuwafariji wanaanza kuwasema kwenye mitandao.

Kuhusu wabunge wa CHADEMA ambao hawahudhurii vikao vya Bunge, Spika Ndugai amesema kesho (leo) atapiga mstari kwa wabunge wote wa chama hicho na atatangaza majina walioitikia wito wake.

Amesema msimamo wake upo pale pale wabunge ambao hawatatii amri ya kurejea bungeni warejeshe hizo fedha na pamoja na kuwasilisha vyeti vya vipimo kuonesha hawana maambukizi ya Corona.