January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHADEMA yataka wananchi wajitetee dhidi ya umasikini

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA)Kanda ya Magharibi kimewataka wananchi kujitetea dhidi ya umasikini kwa kupiga kura katika masuala ya msingi juu ya maisha yao.

Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho kanda ya magharibi, Masanja Katambi akizungumza Septemba 2, 2024 na Waandishi wa Habari amedai uhusiano wa siasa na umasikini wa watu nchini unatokana na sera za serikali kutokutekelezeka na usimamizi duni wa rasilimali.

Akiwa katika ofisi ya CHADEMA Mkoa wa Katavi, Mbali ya kuwasihi wananchi kupiga kura juu ya masuala ya msingi ya maisha yao Kiongozi huyo ametoa wito  kuepuka rushwa inayo ‘baka’ haki, kutweza utu wao kinyume cha Katiba na sheria na kufanya uchaguzi bidhaa.

“Siasa ni maisha kwa kuwa mihimili yote ya utawala inaongozwa na wanasiasa” Amesema Masanja akifafanua umasikini katika nchi yoyote, Watu kukosa huduma za jamii Maji safi na salama, huduma mbovu za afya na miundombinu korofi ya barabara na madaraja wakulaumiwa sio Mhandisi,Mwalimu au Mtaalamu yeyote bali wa kulaumiwa ni mwanasiasa.

Masanja ameweka wazi kuwa mwanasiasa sio mtunga sera za kimaendeleo pekee bali ndiye anayepanga mafungu ya fedha na kuyasimamia hata kama ataweka wataalamu wa TRA lakini wataalamu hao wanasimamiwa na wanasiasa hivyo mtu anapocheza na siasa wanachezea maisha yao.

“Wananchi wajue siasa ndio maisha yao na hakuna eneo lingine la kumwajibisha mwanasiasa. Kumwajibisha Mhandisi anayefanya shughuli zako inawezekana kupitia siasa kwa kupiga kura sahihi” Amesema.

Amesisitiza “Utakapo mchagua Mwenyekiti sahihi wa mtaa/kijiji/kitongoji hao ndio watakao kwenda kuunda eneo la utawala la kamati ya maendeleo ya kata na hao watampangia cha kufanya mtendaji wa kata anayekaa pamoja na Mkurugenzi, Mkurugenzi anayekaa pamoja na wanasiasa ambao ni madiwani na mwenyekiti wao wa halmashauri/Meya ambalo ni jopo la wanasiasa ambao siasa ni utawala wa watu”

Amefafanua kuwa miaka ya 1990 hususani baada ya uhuru wa Afrika Kusini alifika kwenye taifa hilo na kuona utajiri mkubwa uliopo unatokana na mpangilio mzuri wa kisiasa licha ya kuwa mapungufu hayawezi kukosekana.

“Mpangilio mzuri wa kisiasa umelifanya taifa la Afrika Kusini kupiga hatua ya maendeleo kwa sasa ni moja ya mataifa ya Afrika yenye uwezo wa kutengeneza ndege zao za kivita” Amesema Masanja.

Makamo Mwenyekiti huyo, Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya Waziri wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa kutangaza Novemba 27, 2024 itakuwa siku wa uchanguzi wa serikali za mitaa Tanzania bara amesema kupitia Azimio la Mtwara la CHADEMA wamejipanga kuweka wagombea katika maeneo yote nchini.

Amesema kupitia 4Rs za Rais Samia Suluhu Hassan licha ya kuwa yanaweza kutokea mapungufu kwenye uchanguzi lakini wamejipanga kuweka wagombea wenye sifa ya kuwatumikia wananchi kwa maslahi ya maendeleo ya watu na taifa.