January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHADEMA yasikitishwa mawakala wao kuzuiliwa

Na Ashura Jumapili TimesMajira Online,Kagera

Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ), Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera,wamesikitishwa na baadhi ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kuwazuia mawakala wake kuingia katika vituo hivyo wakati wapo kwa mujibu ya sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa chama hicho Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Chief Kalumna,wakati akiongea na vyombo vya habari baada ya kumaliza kupiga kura katika kituo cha Kyaya Kata Kahororo.

Kalumna,amesema baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mawakala hao ya kuzuiwa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura cha Kyaya, alifika eneo hilo na kumtaka msimamizi wa kituo hicho kuwaruhusu mawakala wa CHADEMA kuingia kwa sababu wapo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ndiyo maana waliapishwa kwaajili ya kusimamia jukumu hilo la upigaji kura katika uchaguzi huo.

“Sijui kwa muda waliozuiliwa kuingia kuna mambo gani yalikuwa yanaendelea, inawezekana walikuwa wanaweka kura ambazo wameshazipiga wenyewe wakati mawakala wakiwa nje,”amedai Kalumna.

Amesema pia vituo vya Bugashani Kata Buhembe na kituo cha ofisi ya Kata Kashai mawakala wa CHADEMA walizuiliwa kuingia kitu ambacho kikawaida sio sahihi.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umemalizika leo,tunajifunza kutokana na makosa tunatakiwa kupata Katiba mpya yenye kipengele cha Tume Huru ya Uchaguzi,ili Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,hii mifumo iwe imebadilika kwa sababu kila hatua tuliyopitia vyama vya upinzani tumepata matatizo ikiwemo kuenguliwa kwenye nafasi mbalimbali za kugombea na mawakala kuzuiwa kuingia kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura bado tunaona hatari kwenye kutangaza matokeo ,lazima tuwe na watu wanaosimamia uchaguzi nje ya mfumo wa serikali,”amesema.

Amesema Tawala za mikoa na serikali za mitaa ( TAMISEMI ) hawapaswi kushiriki katika uchaguzi kwa sababu wao ni Wizara na Waziri ni wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),ameteuliwa kutokana na chama chake.

“Tungependa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi wapatikane wakiwa huru, wasiwe na muunganiko wa vyama vya siasa.Ili uchaguzi usiwe na lawama nyingi watu wamekata tamaa,wengine hawajajitokeza kupiga kura kwa sababu wagombea wao wameondolewa bila sababu za msingi,”amesema Kalumna.

Hata hivyo amesema,ameona dosari katika zoezi hilo la upigaji kura kwenye vituo la mpangilio wa majina yaliyobandikwa kwa kutokufuata utaratibu wa mpangilio wa kiherufi,hali ambayo inaweza kusababisha baadhi ya wananchi kushindwa kupiga kura kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta jina lake.

Amesema CHADEMA,kati ya mitaa 66 ya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba waliweka wagombea 63 nafasi ya Uwenyekiti na wajumbe wake wote lakini waliwekewa pingamizi mitaa 23 baada ya rufani walirudishwa wagombea 5 hivyo kuwa na mitaa 39 kati ya 66 iliyopo.