November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHADEMA Jimbo la Segerea yawasilisha Rufaa kupinga wagombea wake kuenguliwa

Na Bakari Lulela, TimesMajira Online

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA) jimbo la Segerea kimewasilisha rufaa ya kuenguliwa kwa wagombea wake wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, Mwaka huu.

Akizungumza Novemba 11,2024 na Waandishi wa habari mara baada ya kuwasirisha rufaa hiyo kwa msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Ilala, Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Segerea ambaye pia ni muweka Hazina wa chama hicho Kanda ya Pwani ,Patrick Asenga amesema kuwa wagombea wa upinzani wameenguliwa kwa hoja zisizo za msingi.

“Tumekuja hapa tangu asubuhi katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Ilala kuna wagombea wetu wa nafasi mbalimbali za uenyekiti wameenguliwa wengi sana kwa sababu zisizo za msingi” amesema Asenga.

Nakufafanua kuwa”Kuna Mgombea ni mwalimu mkuu mstaafu wamemuengua baada ya kujaza kwenye fomu kuwa ni mwalimu mstaafu na kipato chake ni ile pensheni anayolipwa sasa wanamkata kwa madai eti hana kazi ya kufanya”.

Asenga ameendelea kusema kuwa wengine ni wagombea ambao ni wajasiliamari wamekatwa majina yao huku akihoji kwanini wagombea wa CCM ambao ni wajasiliamari hawajakatwa majina yao,nakwamba waliokatwa wote ni wagombea wa upinzani.?

” Hii michezo ya kucheza na Demokrasia namna hii ndiyo michezo ya hivyo,tumewasirisha rufaa yetu mategemeo na matarajio yetu tunamtaka msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Ilala arejeshe wagombea wote wa CHADEMA asikatwe hata mgombea mmoja ili twende tukakutane kwenye sanduku la kura” amesema

Aidha amesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Taifa ,amejipambanua kutumia 4R ikiwa lengo ni kurejesha demokrasia nchini, hivyo wanashangaa vitendo vinavyoendelea vya kuenguliwa wagombea wa upinzani hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.