December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHADEMA ilivyomshauri Rais Samia sakata la Ngorongoro

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemshauri Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kutafuta suluhu ya mgogoro wa wa Wamasai wa Ngorongoro ili kumaliza suala hilo kwa kuangalia umuhimu wa hifadhi ya Ngorongoro na wananch kwa ujumla

Ushauri huo umetolewa hivi karibu jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, wakati akizungumza na waandishi wa habari . Baada ya kauli hiyo siku moja baadaye, Rais Samia alitua wasaidizi wake, wakiongozwa na Waziri William Lukuvi, ambao waliweza kutoa maelekezo mbalimbali ambayo walielekezwa na Rais na wananchi kuridhia.

Rais Samia pia amepanga kwenda kukutana na wananchi hao kupitia viongozi wao.

“Sisi CHADEMA tunaitaka Serikali kukaa chini na wakazi wa Ngorongoro, na kuona namna ya kumaliza changamoto zilizopo eneo hilo badala ya kutumika kwa nguvu,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema Rais Samia kama mfariji mkuu kuwasikiliza wananchi wa Ngorongoro pamoja na kuwarejeshea huduma za kijamii.

“Rais Samia akiwa mfariji mkuu, atumie mamlaka yake kurejesha haki za raia kwa wananchi wa Ngorongoro.” alisema mbowe na kudai kwamba kuna tangazo la kufuta kata, vijiji na vitongoji Ngorongoro, hivyo wao wanapinga hatua hiyo na wanaungana na wengine wote wanaopinga hilo.

Alisema Katiba ya Tanzania imeonyesha nama haki zinavyoheshimiwa ikiwemo haki ya kuishi ,haki ya kusikilizwa na kutokutweza .

Alisema Serikali irudi katika meza ya majadiliano kuzungumza na wananchi wa Ngorongoro,kwani watu hao wana haki zote za msingi kama kuwahamisha wahamishwe kwa ridhaa yao na ushawishi watakaopewa lakini sio kwa kutumia nguvu za vyombo vya ulinzi na usalama.

Alisema wamasai hao wa ngorongoro ni raia halali wenye maeneo halali ya asili yanayopaswa kuheshimiwa,kuenziwa pamoja na kuwa na utajiri mkubwa wa wanyamapori unaozunguka maeneo yao.

”Imetoka amri ya vyombo vya Serikali eti Waziri kufuta Kata,Vijiji,na Vitongoji katika tarafa ya Ngorongoro kwamba sio raia wako ni wageni, hawana haki yoyote hadi kijiji kinafutwa,hii inamaana inafutwa na huduma zote za kijamii haiwezi kupata sio elimu,afya, maji,wala kujengewa barabara na kupewa chochote na serikali.

”Sisi kama Chama tunapinga kufutwa kwa vijiji hivi na tunaungana na Wanasheria kama TLS kama walivyosema wataenda katika vyombo vya dola,mahakama kuelezea jambo hili,Ssi kama chama tutaungana nao katika jambo hili katika kutafuta haki kwa watu wa ngorongoro,”alisema Mbowe.

Aidha aliitaka Serikali bila kujali lini suluhisho la mwisho litapatikana katika sakata la kuhama kwa watu hao wa Ngorongoro kwa haraka lilejeshe huduma za jamii kwa raia hao ,ikiwemo kurudishwa kwa Matibabu na kupeleka dawa kwa Wamama na Watoto.

”Huu ni mkakati wa kufuta jamii fulani hata kama unamgogoro na watu… wafungwa gerezani wanapewa matibabu na wanapewa chakula,tunataka serikali irejeshe haraka huduma za kijamii kwa jamii yote ya Ngorongoro,”alisisitiza.

Mbowe alisema pamoja na hayo pia Mamlaka ya uchaguzi zinapaswa kurejeshe haraka haki za wananchi wa Ngorongoro kushiriki michakato yote ya kupata viongozi ya kuchagua na kuchaguliwa ili kupata viongozi wao.

Alisema hata kama kuna mgogoro katika eneo hilo lakini mgogoro huo hauwezi kuisha kwa kuwanyima watu haki zao za msingi ,ambapo haki hizo haziwezi kuepukika kwa chochote kile hususan katika haki za msingi.

Agosti 18, 2024, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kupitia taarifa kwa umma, ilisema hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na shughuli za utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zinaendelea kama kawaida.

Taarifa hiyo ilizidi kusisitiza kwamba maandamano yaliyoripotiwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii yanaidhihirishia dunia na jumuiya za kimataifa, vyombo vya habari na asasi za kimataifa, kwamba ndani ya hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi.

“Mamlaka inawahakikishia watalii wote waliopanga safari za kuja Ngorongoro kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama wao wakati wote watakapokuwa ndani ya hifadhi,”ilisema taarifa hiyo.