July 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CEOrt inavyopambana kuibua vipaji vya uongozi nchini Tanzania

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

“KUHITIMU Programu hii ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program – CAP), ni deni kwa watu ninaowaongoza na jamii nzima ya Watanzania.”

Hiyo ni kauli ya Anna Shanalingigwa ambaye ni mmoja wa wahitimu 16 wa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Jukwaa la Taasisi ya Wakurugenzi na wamiliki wa makampuni binafsi nchini (CEOrt).

Mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwawezesha Watanzania kushika nyadhifa za juu za Uafisa Mtendaji Mkuu (CEOs) na Ukurugenzi Mtendaji (MDs) katika makampuni na taasisi mbalimbali, tayari yamewanufaisha wahitimu watatu akiwamo Anna Shanalingigwa.

Anna ambaye amehitimu Januari mwaka huu, alipandishwa cheo katika kipindi cha mafunzo hayo na kuwa Kaimu Meneja Mkuu wa Asasi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo – PASS.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Anna anasema ili kufikia malengo hayo ya kushika nyadhifa za juu za Uafisa Mtendaji Mkuu (CEOs) na Ukurugenzi Mtendaji (MDs), kunahitajika nguvu za ziada.

Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson akiwa katika mahafali ya wahitimu wa Programu ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program).

“Kwa sababu mwanamke hata kama una ufaulu mzuri kiasi gani kwenye masomo, kuna nafasi ya mama na mke ambayo jamii inakutegemea uishikilie,” anasema.

Anasema mwanamke anahitaji mkono kutoka kwa wanaume, wafanyakazi na viongozi wake ili awe kiongozi bora kwa manufaa ya kampuni na jamii kwa ujumla.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na mhitimu mwenzake, Rayson Foya ambaye ni Mkuu wa idara ya uchumi katika benki ya Standard Chartered ambaye anasema mafunzo hayo yatamwezesha kujiamini na kushindana katika nafasi za juu ambazo zimekuwa changamoto kwa Watanzania kuzipata.

Mbali na Anna ambaye amepandishwa cheo baada ya kupata mafunzo hayo, Anael Samuel amepandishwa cheo na kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Songas, ilihali, Julius Ruwaichi naye akipandishwa cheo na kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Access Bank.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Chuo cha Strathmore Business School (SBS) , yamefanyika kwa muda wa miezi 12 na kushirikisha CEOrt.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akimtunuku cheti Anael Samuel ambaye ni mmoja wa wahitimu katika mahafali ya Programu ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program). Kushoto ni Sanjay Rughani Mwenyekiti wa Jukwaa la Taasisi ya Wakurugenzi na wamiliki wa makampuni binafsi nchini (CEOrt) ambalo liliandaa mafunzo hayo kwa washiriki 16.

***WAZO LA KUANZISHA MAFUNZO

Aidha, Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania – CEOrt, Sanjay Rughani, anasema wazo la kuanzisha mafunzo hayo lilitokana na utafiti ambao waliufanya na kubaini kuwa makampuni mengi yangependa kuwa na watendaji wakuu Watanzania, lakini hakuna wenye sifa.

“Baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 60 ya viongozi wa kampuni mbalimbali wenyewe walitaka Watanzania na Waafrika wamiliki hizi nafasi za mkurugenzi mtendaji, lakini kuwapata hawa Ma-CEOs ilikuwa kazi ngumu sana,” anasema.

Rughani ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, kabla ya utafiti huo alibaini kuwa benki hiyo yenye umri wa zaidi ya miaka 98, haikuwahi kuongozwa na ofisa mtendaji mkuu kutoka Tanzania.

“Ndipo nilipozungumza na Mwenyekiti wa CEOrt aliyenitangulia, Hayati Ali Mufuruki, tukafanya utafiti huu katika nchi nne na kuja na wazo hili la kuanzisha mafunzo haya hapa nchini,” anasema.

Anasema mafunzo hayo pia yamelenga kuwajengea wataalam wa Kitanzania uwezo mkubwa ili waweze kushindana katika kuhudumu kwenye nafasi za utendaji mkuu katika taasisi, programu na miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa.

“Katika programu hii washiriki 16 ambao wamehitimu, wametoka kwenye kazi zao kama za ofisa rasilimali watu na nyingine lakini watatu kati yao wamepandishwa cheo na kuwa Ma-CEOs katika makampuni ya Songas, PASS na Access Benki.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program) wakiwa katika picha ya pamoja.

“Kwa kweli nina furaha kubwa kwani nilikaa tangu siku ya kwanza ya mafunzo na sasa wanaweza kuzungumza mambo ya kidunia, kisera, kiuchumi na kuwezesha kampuni kupiga hatua.”

***MAJALIWA AWAPA MBINU KUIBUA WATANZANIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye aliwatunuku vyeti wahitimu hao katika mahafali hayo ya kwanza, pia anatoa wito kwa bodi ya wakurugenzi wa CEOrt kushirikiana na serikali pamoja na taasisi nyingine ili kubaini maeneo yenye uhitaji wa viongozi wakuu wazawa na kutoa mafunzo yenye tija.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akimtunuku cheti Sarah Majengo ambaye ni mmoja wa wahitimu katika mahafali ya Programu ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program).

Anasema ni vema bodi hiyo ikajipanga kuandaa mipango ya mafunzo yenye lengo la kutambua na kujenga uwezo kwa Watanzania katika sekta za kipaumbele hususani sekta ya madini, mafuta na gesi, ujenzi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Pia Waziri Mkuu anasema ushirikiano wa CEOrt pamoja na Taasisi ya Uongozi inayoendesha programu za mafunzo ya uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Alto cha Nchini Finland, utaleta tija, kuondoa marudio na kuimarisha ubunifu katika kutoa mafunzo na kuleta manufaa kwa washiriki wa mafunzo hayo.

“Huu ni muda muafaka kwa CEOrt kushirikiana katika kuwajengea uwezo wa wataalam wabobezi katika masuala ya uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa CEOrt pamoja na wahitimu katika mahafali ya Programu ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program).

Mafunzo haya yamekuja katika wakati muafaka kwani yanaendana na falsafa ya Serikali ya awamu ya tano ya ‘hapa kazi tu’, pia yamekuja katika kipindi ambacho nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo viongozi hao watumie ujuzi na weledi katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu, rasilimali fedha na miradi,” anasema Majaliwa