December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCWT yamchangia milioni moja,Rais Samia kwa ajili ya fomu ya kuwania Urais 2025

Na Lubango Mleka, Times majira online – Igunga.

CHAMA Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimemchangia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kiasi cha milioni moja kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuwania Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) uchaguzi ujao wa 2025.

Fedha hizo zimetolewa na wanachama wa chama hicho katika kongamano lao linaloendelea katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine wilayani Igunga mkoani Tabora na kuhudhuriwa na zaidi ya wafugaji 3000 kutoka Kanda nane hapa nchini.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Mrida Mshota akizungumza katika kongamano la chama hicho wilayani Igunga

Akizungumza katika kongamano hilo Mwenyekiti wa CCWT Mrida Mshota amesema kuwa, wametoa fedha hizo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia za kuleta Maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwatambua wafugaji jambo ambalo limechochea kukua na kuongeza wawekezaji katika sekta hiyo.

“Toka tumeingia madarakani mimi na wenzangu tulikuta migogoro na changamoto nyingi lakini kwa miaka hii mitatu bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilikuwa bilioni 166 lakini mwaka huu Wabunge wamepitisha bilioni 460,sasa muone serikali ilivyofanya kazi, wafugaji tusikae kama mabubu tuseme mambo ambayo Rais ametufanyia kwa maendeleo yetu,”amesema Mshota.

“Tunamuunga mkono na tunampa miaka mingine mitano tena na leo tunatoa milioni moja kumchukulia fomu na tutaendelea kuchanga zaidi kufanikisha anashinda kwa asilimia 96.6 kwa hali na mali,”amesema Mshota.

Naye Mlezi wa chama hicho Taifa Joseph Makongolo amesema kuwa Serikali imetatua matatizo ya wafugaji kwa kiwango kikubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha akizungumza katika kongamano la Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT)

Hivyo amemuomba Rais Dkt. Samia kuongeze maeneo kwa wafugaji na mabwawa yanayochimbwa kwa ajili ya maji kuwekwe mabirika ya kunyweshea ng’ombe.

“Wafugaji wenzangu dumisheni amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu jambo hili litamrahisishia Rais na viongozi wake kufanya kazi kwenye suala letu la ufugaji na kupata ufugaji wenye tija,”

Sanjari na hayo amewaomba wafugaji kusitisha migogoro na wakulima kwani wote ni watoto wa baba na mama mmoja.

“Kwa asilimia fulani sisi ndio tumekuwa chanzo cha migogoro ya mipaka ambayo imezuiwa naomba tuache migogoro kwenye maeneo yasiyo yetu,” amesema Makongolo.

Naye mmoja wa wafugaji na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata maziwa ya ng’ombe cha Kahama Fresh Jossam Ntengeki amesema kuwa ameamua kuwekeza nchini kutokana na kuisha kwa migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.

Hivyo amaanzisha kiwanda cha kuchakata maziwa mkoani Kagera na sasa anaangalia namna ya kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama hapa nchini Mkoa wa Tabora hasa wilayani Igunga na baadae atajenga kiwanda cha kuchakata ngozi.

Mlezi wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Joseph Makongolo akiwaasa wafugaji nchini kuacha migogoro na wakulima ikiwa ni pamoja na kutokuingia katika ardhi ambayo imepangwa kwa matumizi yasiyo ya wafugaji katika kongamano la chama hicho linalofanyika wilayani Igunga

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha amesema kuwa, amepokea maoni ya wafugaji nchi nzima kupitia kongamano hilo na amepokea fedha hizo na atampelekea Rais Dkt Samia ikiwa ni pamoja na kufikisha salamu zao za kumuunga mkono katika uchaguzi ujao.

Ameongeza kwa kusema kuwa, kila litakapo jengwa bwawa la maji zitajengwa sehemu za kunyweshea ng’ombe na kila eneo litakapo pita bomba la maji kutoka Ziwa Victoria wataweka sehemu za kunyweshea.

Wafugaji kutoka Kanda nane hapa nchini wakiwa katika kongamano la Chama Cha Wafugaji Tanzania linalofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine uliopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Igunga