November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM,yafanya dua kumuombea marehemu Kibao

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa Tanga, kimefanya dua maalumu ya kumuombea marehemu Ali Kibao aliyekuwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA).Ambaye aliyefariki hivi karibuni baada ya kutekwa na watu wasiojulikana na kisha kuuwawa,na mwili wake kutupwa kwenye eneo la Union jijjni Dar-es-Salaam.

Dua hiyo ya kumuombea marehemu Kibao,imefanyika Septemba 19,2024,katika msikiti wa Ijumaa jijini Tanga.Huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga, Rajab Abrahaman Abdallah, ameungana na watanzania wengine kulaani vitendo vya baadhi ya watu kutekwa na kuuwawa kikatili.

“Tumeguswa na msiba huu,tunaungana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na watanzania wengine, kwamba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini wale wote waliohusika na mauaji hayo,”amesema Abdallah.

Sanjari na hayo Abdallah,ametumia fursa hiyo, kuwahimiza Watanzania kukemea, kufichua matendo maovu na ya kihalifu,yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.Ambapo matukio hayo yamekuwa yakileta madhara kwa jamii.

“Mara nyingi nchi yetu,kuna vipindi vigumu inapitia,mtakumbuka miaka ya nyuma kidogo, kulikuwa na wimbi la mauaji ya watu wenye ulemavu (Albino),kutokana na watu kudanganywa na waganga,kuwa ukiwa na kiungo cha Albino wewe ni tajiri,kumbe sio kweli ni ukatili tu ulikuwa ukifanyika,”amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Japhari Kubecha, ameishukuru Familia ya marehemu kwa kuridhia kufanyika kwa dua hiyo.Huku akisisitiza kuwa serikali ya Mkoa Tanga, itaendelea kupambana na uhalifu wa aina yeyote ili kuhakikisha wananchi wanaishi mahala salama pamoja na mali zao.

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Mkoa Tanga,Juma Luwuchu, amewaasa wanafamilia kuendelea kuwa na subira, katika kipindi chote ambacho uchunguzi unaendelea kufanyika, ili kubaini waliohusika na uhalifu huo.

Akuzungumza kwa niaba ya familia ya marehemu Ali Kibao, mmoja wa familia hiyo Mukhusin Hemed ameishukuru serikali kwa kuungana nao katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.