Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mwenyekiti wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kimezindua rasmi Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa leo Mei 29, 2025 Jijini Dodoma unaohudhuriwa na wajumbe 1907 sawa na asilimia 98.6.
Akizindua mkutano huo, Mwenyekiti huyo amezitaja ajenda za mkutano huo kuwa ni pamoja na Marekebisho madogo ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la Januari 2025, kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kwa kipindi cha miaka mitano pamoja na kuzindua Ilani ya CCM itakayotumika katika uchaguzi mkuu 2025.

Pia katika mabadiliko ya katiba ya chama ameyataja kuwa ni pamoja na baadhi ya vikao vya mikutano ya chama hicho kufanyika kwa njia ya mtandao endapo kutakuwa na ulazima na kwa kuzingatia katiba ya chama hicho ikiwemo kikao cha Kamati kuu na Halmashauri kuu, huku akivitaja vikao husika kwa ngazi ya wilaya na Mkoa endapo vitahitajika kufanyika kwa njia ya mtandao vitatolewa ruhusa na Katibu Mkuu.
Aidha, ametaja mafanikio ya chama hicho kuwa mbali na idadi ya usajili wa wanachama hadi sasa kufikia 13,000,670 mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa jengo la chama ambalo litajengwa Jiji Dodoma na kugharimu zaidi ya Sh. Bil 30, ambapo jengo hilo linatarajiwa kukamilika mnamo 2027 likiwa na njia rafiki kwa watembea kwa miguu, chem chem ya kupooza makali ya jua, sehemu ya kupigia picha, sehemu ya kutua helikopta itakayotumiwa na Mwenyekiti, Katibu na wageni maalumu pekee, maegesho ya magari, ukumbi wa mgahawa wenye sehemu ya chini na juu maktaba na ukumbi wa mikutano.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, akizungumzia mafanikio ya mkutano huu, amesema idadi ya uhudhuriaji ya mkutano huu imekidhi akidi ya mahudhurio ya wajumbe, hivyo kufanya mkutano huo kuwa halali ikiwa pamoja na maamuzi yatakayo hafikiwa katika kikao cha mkutano huo.
Aidha mkutano huo umehudhuriwa na wadau wa vyama mbalimbali vya siasa ndani na nje ya nchi, viongozi wa dini na wawakilishi wa taasisi mbalimbali kiserikali na zisizo za kiserikali.


More Stories
AI Spam Filter na Usalama wa Data Zako
Bodi ya Ithibati yasisitiza Waandishi wa Habari kuweka vyeti vya kitaaluma katika mfumo wa Tai-Habari
REA yahamasisha wananchi kutumia Mkaa Mbadala