Na Suleiman Abeidi,Timesmajira Online, Shinyanga
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Shinyanga kimewatoa hofu wananchi kutokana na changamoto ya ukosefu wa baadhi ya huduma katika Hospitali mpya ya Rufaa iliyopo eneo la Mwawaza Manispaa ya Shinyanga.
Baadhi ya huduma zinazodaiwa kukosekana katika hospitali hiyo ya rufaa ni pamoja kutokuwepo kwa jengo la kuhifadhia maiti na chumba cha picha za mionzi (X-Ray) na kwamba kukosekana kwa huduma hizo kunawasababishia usumbufu mkubwa wananchi.
Hata hivyo katika hotuba yake kwa wananchi wa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Mabala Mlolwa amewatoa hofu wananchi kwa kuwaeleza kuwa huduma zote muhimu zitaanza kupatikana kwenye hospitali hiyo kuanzia mwezi Julai mwaka huu.
Mlolwa amesema mara baada ya kuanza kutumika rasmi kwa hospitali hiyo ya rufaa baadhi ya majengo yalikuwa hayajakamilika lakini hivi sasa tayari mambo yote yameisha kamilika na huduma zote za matibabu ikiwemo jengo la kuhifadhia maiti (mochwari) zitapatikana hospitalini hapo kuanzia mwezi Julai mwaka huu.
“Ndugu zangu naomba niwahakikishie kwamba zile changamoto zilizokuwepo katika hospitali yetu mpya ya Rufaa kule Mwawaza hivi sasa zimefanyiwa kazi na huduma zote muhimu zitaanza kupatikana kuanzia mwezi ujao wa Julai mwaka huu,”ameeleza na kuongeza kuwa
“Hivyo basi ondoeni hofu na msiwe na wasiwasi tena, maana Serikali yenu ya awamu ya sita ina dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi kama ilivyoelezwa ndani ya Ilani yetu ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020, miongoni mwa ahadi hizo ni suala la kuboresha afya za watanzania kwa kuhakikisha wanapata huduma za uhakika za matibabu,” ameeleza Mlolwa.
Mbali ya huduma za kimatibabu lakini pia Mlolwa amesema kwa upande wa suala la barabara inayotoka maeneo ya mjini kwenda kwenye hospitali hiyo inayodaiwa ni mbovu kutokana na kuwa ya vumbi tayari mipango imo mbioni kuhakikisha barabara hiyo inawekewa lami.
“Serikali yetu ya awamu ya sita inastahili pongezi kubwa, tulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya za uhakika na mara nyingi watu walilazimika kwenda kutibiwa Bugando Mwanza, lakini sasa huduma hizo zitapatikana hapahapa kwenye hospitali yetu,”
“Suala la changamoto ya barabara ya vumbi linafanyiwa kazi, na hivi karibuni mtaona barabara hiyo inaanza kuwekewa lami na itarahisisha zaidi usafiri wa kwenda kwenye hospitali yetu hii kubwa, na tuwaombe watanzania waendelee kukiamini Chama cha Mapinduzi ambacho ndiyo pekee chenye sera nzuri,” ameeleza Mlolwa.
Katika uwasilishaji wa kero mbalimbali zinazowakabili baadhi ya wananchi wamelalamikia ukosefu wa baadhi ya huduma kutopatikana katika hospitali ya rufaa ikiwemo kutofanya kazi kwa hospitali ya Manispaa ambayo ingeweza kuwapunguzia wazee tatizo la kutembea umbali mrefu kufuata matibabu kwenye hospitali ya rufaa.
Kwa upande wake Robert Ngh’welo mkazi wa Kata ya Ndembezi amesema moja ya changamoto inayowakabili wazee ni kutembea umbali mrefu kilometa sita kwenda hospitali ya Rufaa iliyopo Mwawaza na kwamba nauli kwa Bajaji ni shilingi elfu tatu ambapo ni elfu sita kwa kwenda na kurudi.
“Mwenyekiti ombi letu kwako ni sisi wazee kuhurumiwa, hii hospitali ya Rufaa iko mbali, hivyo ni vyema ilipokuwa hospitali yetu ya Mkoa, sasa itoe huduma kama hospitali ya Wilaya, ili wananchi tupate huduma pale badala ya kulazimika kwenda Mwawaza, ni mbali na huduma nyingine kule hakuna,” ameeleza Ngh’welo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Elisha Robert amesema tayari mipango ipo mbioni ya Manispaa kukabidhiwa majengo ya iliyokuwa hospitali ya Mkoa ili yaweze kutumika kama hospitali ya Wilaya na huduma zinatarajiwa kuanza kutolewa mapema mwezi Julai mwaka huu.
“Ni kweli hivi sasa wagonjwa wengi wanalazimika kwenda katika hospitali yetu ya Mwawaza, hii inatokana na kuwepo kwa marekebisho kwenye majengo ya iliyokuwa hospitali ya mkoa, niwahakikishie wananchi wetu tayari taratibu za Manispaa kukabidhiwa majengo ya hospitali hiyo zimekamilika pia ujenzi wa baadhi ya majengo muhimu upo mbioni kukamilika, tunatarajia huduma zitaanza kupatikana rasmi mwezi Julai mwaka huu,” ameeleza Dkt. Robert.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi