Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,odoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza vipaumbele tisa vya Ilani yake ya Uchaguzi kwa mwaka 2025–2030, ambayo itatumika kunadi sera zake kwa wananchi katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Ilani hiyo imewasilishwa leo Mei 30, 2025, jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya CCM, Prof. Kitila Mkumbo, katika Mkutano Maalum wa chama hicho uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
Prof. Kitila alisema Ilani hiyo ni ya saba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, na imetokana na uchambuzi mpana wa maoni ya wananchi, wanachama wa CCM, asasi za kiraia, wasanii, na wadau mbalimbali kutoka pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tumezingatia maoni ya Watanzania kuhusu changamoto zinazowakabili, hasa suala la ajira kwa vijana, ili kuhakikisha kuwa Ilani yetu inagusa maisha ya watu kwa njia halisi na thabiti,” alisema Prof. Kitila.
Vipaumbele Tisa vya Ilani ya CCM 2025–2030
Prof.Kitila alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na Kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa – wa aina ya fungamanishi, jumuishi na wa ushindani, unaojengwa katika misingi ya kuongeza thamani ya rasilimali za taifa na kuongeza fursa za ajira kwa vijana, kuinua kipato cha wananchi na kupunguza umaskini.
Vingine ni kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii,kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji,Kukuza na kutumia sayansi na teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kijamii,Kudumisha demokrasia na utawala bora na kulinda amani, utulivu na usalama wa nchi.
Pia Kudumisha utamaduni wa taifa pamoja na kukuza sanaa na michezo,Kuongeza kasi ya maendeleo ya vijijini.
Prof. Kitila amesema Ilani hiyo imejengwa kwa msingi wa matokeo ya tafiti za kisayansi zilizolenga kuelewa matamanio na mahitaji halisi ya Watanzania. Pia imejikita katika mwelekeo wa CCM wa mwaka 2020–2030 wa kujenga uchumi wa kitaifa unaojumuisha sekta za viwanda na huduma.
Akizungumzia kuhusu uchumi wa buluu, Prof. Kitila alieleza kuwa CCM itaielekeza Serikali kuchukua hatua 11 muhimu, ikiwa ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mitaji, mikopo na vifaa kwa wavuvi na vyama vya ushirika, pamoja na kuanzisha bandari za uvuvi katika maeneo ya Bagamoyo na Kilwa, na kuimarisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kama zao la kiuchumi na lishe.
“Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza mwaka 1995, CCM imeendelea kuongoza kwa dira ya kuijenga Tanzania inayozingatia utu, haki, usawa na kuheshimika kimataifa,” alisisitiza Prof. Kitila.
Zanzibar Yajumuishwa kwa Vipaumbele Maalum
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema kuwa kwa upande wa Zanzibar, Ilani hiyo inajumuisha vipaumbele 13 vinavyolenga kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku kipaumbele kikiwa ni kuimarisha mshikamano, umoja na maridhiano.
“Tunalenga kuzalisha ajira zaidi ya 350,000 kwa vijana kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi, huku tukihakikisha kuwa miradi ya maendeleo inaendana na hali halisi ya Wazanzibari,” alisema Dkt. Saada.
Aidha, alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana Zanzibar hadi sasa ni matokeo ya hali ya amani, mshikamano na utulivu, hali ambayo CCM inakusudia kuendeleza katika kipindi kijacho.
More Stories
TAKUKURU yanasa watuhumiwa wa wizi wa mali za wakulima
CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa tuzo na Bunge
Mwenge wazindua Miradi saba Temeke