November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yatanabaisha maendeleo ya mwaka mmoja wa Rais Samia 10

Na David John, TimesMajira Online

KATIBU mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Daniel Chongolo amewatoa hofu watu wanaodhani kuwa rais Samia Hassan Suluhu kuna mtu nyuma yake ambaye anamwendesha.

Amesema kuwa watu wanatakiwa watambue kuwa urais ni taasisi na wala si mtu hivyo hakuna mtu ambaye anaweza kuwa nyuma ya rais Samia na kumpangia nini chakufanya kama mnavyofikiri.

Chongolo ameyasema haya leo katika ofisi ndogo za Chama cha Mapinduzi Lumumba Dar es Salaam wakati akizungunza na waandishi wa habari kuhusu mwaka mpya wa serikali ya awamu ya sita ya rais Samia Suluhu.

” Nataka niwaeleze kuwa hakuna mtu ambaye anaweza kumuongoza rais na lazima mtambue kuwa urais ni taasisi na wala siyo mtu kama mnavyofikiria na kwa taarifa yenu kauli yake ni utekelezaji.” amesema Chongolo

Katibu huyo amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali na mmoja waandishi wa habari kuwa kunasemakana rais Samia yuko mtu ambaye yuko nyuma yake ndio anayemuongoza kuhusiana na utendaji wake wa kila siku.

Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita chini ya rais Samia Suluhu Katibu Chongolo amesema kuwa tangu rais Samia apokee kijiti hicho kutoka kwa mtangulizi wake Hayati Rais Dkt John Magufuli ambaye alifariki dunia machi 17 ,2021 amekuwa akifanya kazi kubwa.

Amesema kuwa rais Samia katika kipindi cha mwaka mmoja amefanikiwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/ 25 na chama cha Mapinduzi CCM kimeendelea kuisimamia Serikali kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanafika haraka kwa wananchi.

” Ndugu zangu nyie wenyewe mmekuwa mashahidi na mnaona kazi kubwa ambayo Serikali yetu inafanya hususani na kipindi hiki cha mwaka mmoja ambapo kesho Machi 19/ 2022 rais samia anatimiza mwaka mmoja mengi yamefanyika.”amesema

Amesema karibu maeneo yote yamekuwa na mafanikio makubwa hususani kwenye miundombinu ya barabara serikali imeendelea kukamilisha miradi mbalimbali na mzunguko wa fedha upo na wananchi wanashiriki kikamilifu kwenye shughuli maendeleo.

Pia amesema katika sekta ya Elimu rais Samia amefanya kazi kubwa na katika mwaka huu wa masomo kidato cha kwaza wamefanikiwa kuaza masomo bila kukosa hata mwanafunzi mmoja kwani ameweza kukamilisha ujenzi wa madarasa 15000 nakupelekea watoto wote kwenda shule.

Amefafanua kuwa rais samia ameifungua nchi kwenye medani ya kimataifa na katika hilo amefanikiwa kusaini mikataba mbalimbali ya kimakubaliano kwa ajili ya maendeleo ya wanannchi.

Rais Samia Suluhu kesho anatimiza mwaka mmoja tangu alipopokea kijiti cha urais machi mwaka jana siku mbili tu baada Ya aliyekuwa rais awamu ya tano Hayati Dkt.John Magufuli kufariki dunia na kwa mujibu wa katiba Makamu wa Rais anakula kiapo cha kutwaa madaraka hayo ya urais.na madhimisho hayo.yanafanyika mkoani shinyanga.