Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, imepokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Ilani ya CCM, iliyoambatana na ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo iliyopo katika Wilaya ya Ilala.
Akipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo Novemba 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo pia, ametembelea na kukagua maendeleo ya miradi inayoendelea kujengwa katika wilaya hiyo.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa ghorofa wa Shule ya Sekondari ya Kimanga, yenye madarasa 12 na matundu ya vyoo 27.
Ujenzi wa ghorofa Shule ya Sekondari ya Liwiti yenye madarasa 20 na matundu ya vyoo 46, ujenzi wa ghorofa tatu Shule ya Msingi Diamond na matundu ya vyoo 30, na ujenzi wa madarasa 9 ya Shule ya Msingi Mnyamani.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara ya ‘Boom’ yenye urefu wa Km 0.44 iliyopo Buguruni Mnyamani, iliyojengwa kwa kiwango cha lami, pamoja na kukagua Mradi wa uwekaji wa vigae (Paving Blocks), pembezoni mwa bustani katika barabara ya Luthuli, lengo likiwa ni kuimarisha usafi na kuboresha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa, halmashauri imeanza kutekeleza uboreshwaji maeneo ya pembezoni mwa barabara kuu za mjini kwa kuweka ‘Paving blocks’ katika njia za watembea kwa miguu.
Akihitimisha baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mtenvu, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kuendelea kutekeleza Ilani ya chama, ambapo amesema miradi yote aliyotembelea imeonekana kuwa katika hatua nzuri.
Ameitaka halmashauri hiyo kuwalipa wakandarasi wa miradi kwa wakati ili miradi iweze kukamilika kwa muda uliopangwa na kumtaka Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo kuwachukulia hatua wakandarasi wanaochelewesha miradi hiyo.
“Kwanza niupongeze uongozi wa Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi, mmehakikisha fedha mlizozipokea zinatekeleza miradi kwa ufasaha. Hivyo nimuagize Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kuhakikisha mnalipa wakandarasi kwa wakati na Mkandarasi anayechelewesha mradi achukuliwe hatua”, amesema Mtenvu.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewatoa hofu wakandarasi wote wanaoendelea na ujenzi wa miradi hiyo, kuwa endapo Kuna changamoto zozote wanazokabiliana nazo Serikali ipo tayari kuzitatua ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi