February 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yaombwa kuchunguza vitendo vinavyofanywa na Mwenyekiti wa CCM Rorya

Na Mwandishi wetu,Timesmajira 

KADA  wa  Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Rorya ambaye  aliyewahi kuwa mtumishi wa CCM Makao Makuu Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Baraka Otieno, ametoa rai kwa   Kamati ndogo ya Udhibiti nidhamu  inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara,Steven  Wassira  kuunda timu maalum ya kuchunguza vitendo vinavyofanywa na Mwenyekiti wa Wilaya ya Rorya Ongujo Wakibara cha  kuwagawa Viongozi wa  Chama na Watendaji.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kada huyo  amesema  Mwenyekiti huyo 

amekuwa akiwatishia wajumbe na madiwani kuwa atakata majina yao kama hawatamuunga mkono Mbunge wa sasa wa Jimbo hilo Jafari Chenge.

Amesema Mwenyekiti na Mbunge huyo wamekuwa na tabia ya kuwagawa na kuwabagua viongozi wa Kata na Matawi ambao hawapo katika mlengwa wao jambo ambalo halina afya kwa Chama.

“Viongozi wengi wanaobaguliwa na Mwenyekiti huyo ni wale wanaotoka katika tarafa ya Dirango na baadhi ya kata ya Zuloimbo na Suba.

Amesema Mwenyekiti huyo amekuwa akiagiza viongozi wa chama ngazi ya kata kuwasimamisha viongozi bila kufata katiba wala kanuni za maadili wala kuhusisha kamati ya siasa ya wilaya.

“Tunayazugumza mambo haya ili wanaccm nchi nzima waelewe kinachoendelea wilayani Rorya, kamwe hatuwezi kunyamazia vitendo kama hivi vinavyofanywa na Mwenyekiti  huyu kwani 

imefika mahali rorya wanaccm na wananchi kwa ujumla  wanajiuliza Chama hiki kimetekwa na wafanyabiashara kiasi cha kufanya  matukio ya utovu wa nidhamu na wasichukuliwe hatua,”amesema Otieno 

Aidha amesema wananchi wa Wilaya ya Rorya wanaonesha dhahiri kukichoka chama cha mapinduzi kwasababu ya Ongujo,kutokana na fedha zake anafanya kama anaimiliki CCM,kwani hadi baadhi ya vikao vya CCM ngazi ya Wilaya vinafanyika nyumbani kwake.

”Mwenyekiti huyu anatawaliwa na ubinafsi,CCM ndani ya wilaya ya Rorya ipo kwenye wakati mgumu sana kutokana na ubinafsi huo uliopitiliza wa mwenyekiti huyo anayewagawa wanaccm katika mafungu kutokana na ubinafsi huo.

Amesema kuhusu ukweli,Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ukweli una tabia moja nzuri haujali mkubwa wala mdogo,adui au rafiki kwake watu wote ni sawa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Ongujo Wakibara, amesema hali ya kisiasa ndani ya wilaya hiyo iko shwari japokuwa lipo vuguvugu linalosababishwa na wakati uliopo wa kuelekea uchaguzi mkuu ambao utafanyika baadaye mwaka huu.

Hata hivyo, Wakibara amesema Chama kimesimama imara kuwaunganisha wanachama wote huku pia kikiwalinda viongozi wawakilishi wa wananchi wamalize kipindi chao cha uongozi na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.

“Mimi nikiwa msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika eneo langu naendelea kuwalinda viongozi wa kuchaguliwa akiwemo mbunge, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa wanaotokana na Chama chetu,” amesema.

Pamoja na kuhakikisha viongozi hao wanapewa nafasi ya kuwatumikia wananchi, pia wanachama wote wa CCM wameendelea kupewa fursa ya kukitumikia Chama na muda utakapowadia kila mmoja atapata fursa ya kupambania nafasi za uongozi.

“Kwa sasa tunaowatambua wanatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni mbunge (Jafari Chege), madiwa na viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji, tuwape nafasi wakamilishe ngwe yao katika utekelezaji wa ilani,” amesema.