Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza mshtuko na masikitiko yake makubwa kufuatia tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima, usiku wa Aprili 30, 2025, katika eneo la Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya chama hicho iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Padre Kitima alivamiwa na watu wawili wasiojulikana waliomshambulia kwa kutumia kitu butu kichwani na sehemu mbalimbali za mwili, na kusababisha majeraha makubwa.
CCM imeungana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, kulaani vikali tukio hilo ambalo chama kimelitaja kuwa ni la kikatili, lisilo na utu na lenye nia ya kutishia amani na utulivu wa viongozi wa dini nchini.
“Hili ni tukio la kusikitisha mno dhidi ya mtu ambaye amejitoa maisha yake kuhudumia jamii kwa upendo na uadilifu. Chama kinatoa pole nyingi kwa Padre Kitima, familia yake, TEC, na waumini wote wa Kanisa Katoliki walioguswa na tukio hili,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Chama hicho kimevitaka vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka na za kina kufanya uchunguzi, ili kuwabaini wahusika wa shambulio hilo na kuwafikisha mbele ya sheria bila kuchelewa.
Aidha, CCM imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi zote za kidini katika kuhakikisha taifa linaendelea kuwa nguzo ya amani, mshikamano, heshima na haki kwa wote bila kujali itikadi au imani.
“Tunamuombea Padre Kitima uponaji wa haraka na kurejea salama katika majukumu yake ya kiroho na kijamii,” alihitimisha Balozi Dkt. Nchimbi.
Tukio hilo limeibua hisia kali kutoka kwa wananchi, viongozi wa dini, na mashirika ya kijamii huku wengi wakitaka hatua madhubuti zichukuliwe ili kulinda usalama wa viongozi wa dini na raia wote kwa ujumla.
More Stories
Kibasila wafurahia mafanikio ufaulu asilimia 100 kwa miaka mitatu
DAS Ilala awafunda wahitimu Benjamin Mkapa
Wanafunzi Zanaki watakiwa kulinda heshima ya shule