April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yajipanga Uchaguzi 2025, mchakato wa uteuzi kuanza Mei

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo wanachama wote wanaotaka kugombea Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani wanatakiwa kuchukua na kurejesha fomu kuanzia tarehe 1 Mei hadi 15 Mei 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA. Amos Gabriel Makalla, zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu litaanza saa 2:00 asubuhi na kufungwa rasmi saa 10:00 jioni tarehe 15 Mei, 2025.

Katika utaratibu huo, wanachama wanaotaka kugombea nafasi ya Ubunge au Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wanapaswa kuchukua na kurejesha fomu hizo kwa Katibu wa CCM wa Wilaya anayoishi au anayokusudia kugombea.

Aidha, kwa wale wanaotaka kugombea Viti Maalumu vya Wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na makundi maalumu kama vile NGOs, Wafanyakazi, Wasomi na Watu wenye Ulemavu, watapaswa kuchukua na kurejesha fomu kwa Katibu wa UWT wa Mkoa husika.

Kwa upande wa vijana wanaotaka kugombea Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), fomu zitapatikana kwa Katibu wa UVCCM wa Mkoa, huku wanaotaka kupitia Umoja wa Wazazi wa CCM wakitakiwa kuchukua na kurejesha fomu kwa Katibu wa Wazazi wa Mkoa husika.

Kwa nafasi ya Udiwani, wanachama wanaotaka kugombea Kata upande wa Bara au Wadi upande wa Zanzibar, wanatakiwa kuchukua na kurejesha fomu kwa Katibu wa CCM wa Wilaya husika.

CCM imesisitiza kuwa wanachama wote wanaokusudia kugombea ni lazima wazingatie taratibu na kanuni za chama katika kipindi chote cha mchakato huo, ili kuhakikisha haki, usawa na nidhamu vinaendelea kupewa kipaumbele.

Mchakato huu wa ndani wa chama unatajwa kuwa ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo CCM imejipanga kuhakikisha inapata wagombea bora na wenye sifa stahiki za kuwatumikia wananchi katika nafasi mbalimbali za uongozi.