Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Samia Suluhu Hassan, amehitimisha Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wa siku mbili ulianza Mei 29-30,mwaka huu kwa kutoa wito wa mshikamano, maandalizi ya kina na utekelezaji madhubuti wa ilani ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza wakati akifunga Mkutano huo,Dkt.Samia alisema kuwa lengo kuu la mkutano ni kuhakikisha chama kinajipanga kikamilifu kushinda uchaguzi na kuendelea kuongoza nchi kwa mafanikio.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema kuwa ,Ilani iliyozinduliwa imeandaliwa kwa weledi mkubwa, ikiwa ni nyenzo mahsusi ya kujenga hoja kwa wananchi.
Alitumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri wa Mipango Dkt. Kitila Mkumbo na timu nzima iliyoandaa ilani hiyo kwa kazi nzuri na kukamilisha kwa wakati.
“Ilani hii imesheheni mambo ya msingi, haijaacha kitu, na tunaweza kuyatekeleza yaliyomo,” alisema Rais Samia.
Alibainisha kuwa mafanikio ya utekelezaji wa ilani iliyopita ni uthibitisho kuwa chama kina uwezo wa kutimiza ahadi zake kwa wananchi.
Katika hatua ya kuhakikisha ilani hiyo inatekelezwa kwa ufanisi, Rais Samia aliagiza kutengenezwa kwa vitabu vidogo vya ilani vinavyobeba wajibu wa kila mmoja katika ngazi mbalimbali za chama katika mikoa na wilaya.
Alisema,baada ya kuandaliwa ,Vitabu hivyo visambazwe kote nchini ili kuwezesha kila mwanachama a viongozi katika mikoa na wilaya kuifahamu vizuri ilani na kujua nafasi yake katika utekelezaji.
“Kila mmoja wetu lazima afanye kazi kwa bidii katika nafasi yake,” alisisitiza.
Rais Samia pia alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi kama ambavyo imeainishwa katika ilani hiyo, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Aidha, aliwataka wanachama kuhakikisha wanaitetea, kuihamasisha, na kuwashawishi wananchi kuiunga mkono ilani hiyo kama sehemu ya kulinda maono ya chama
More Stories
TAKUKURU yanasa watuhumiwa wa wizi wa mali za wakulima
CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa tuzo na Bunge
Mwenge wazindua Miradi saba Temeke