November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yaipongeza TARURA ukarabati wa barabara

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Bukoba

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi CCM Ndugu Shaka Hamdu Shaka ametembelea Mradi wa Matengenezo ya sehemu Korofi katika Barabara ya Katoro-Kyamulaile-Kashaba(Kilometa 5)na Izimbya- Katokoro(Kilometa 3.8) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya Bukoba Eng. Maziku A. T. akisoma taarifa mbele ya Mwenezi CCM Taifa amesema
“Lengo kubwa la Mradi huu ni kurudisha Mawasiliano katika Kata hizi na Maeneo ya jirani ambapo wananchi walilazimika kutumia usafiri wa Mitumbwi katika kuendesha Shughuli za Kiuchumi na Kijamii”

Akizungumza baada ya Kutembelea Mradi huo Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi CCM,Shaka Hamdu Shaka ameipongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA chini ya Mtendaji Mkuu wa TARURA Eng Victor Seff kwa namna inatekeleza kwa Vitendo Ilani ya CCM na Maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 imeelekeza katika kipindi cha miaka 5 hii inaenda kuimarisha TARURA na tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya kipindi kifupi TARURA imeongezewa Bajeti kutoka Sh bilioni 273 mpaka Sh bilioni 966 kwa mwaka wa fedha 2021/22.” SHAKA

” Na Wote ni mashahidi TARURA kwa sasa wanafanya kazi nzuri na kuongezewa kwao bajeti na wataalamu ni imani yetu watafanya kazi nzuri zaidi ya hizi, tunawatia moyo endeleeni na Chama kinaunga mkono juhudi hizi” amesema Shaka

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Rumanyika Investment Co. Ltd kwa gharama ya zaidi ya Milioni 519,573,220.00 ambaye ameishatekeleza na kumaliza kazi kwa asilimia 98 na mradi umeanza kutumika kwa kutoa huduma kwa wananchi.